Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imezuia uingizaji wa
soseji kutoka Afrika Kusini zilizobainika kuwa na bakteria aina ya listeria.
Uamuzi wa TFDA unatokana na soseji hizo aina ya Polony kubainika
kuwa na aina hiyo ya bakteria wanaosababisha ugonjwa wa listeriosis
uliosababisha vifo vya watu 180 nchini Afrika Kusini.
Soseji hizo kwa mujibu wa habari zilizochapishwa na vyombo
kadhaa vya kimataifa zinatengenezwa na kiwanda cha tiger brands unit
enterprises na cha RCL foods vyote vya Afrika Kusini.
Waziri wa Afya wa Afrika Kusini, Aaron Motsoaledi alikaririwa na
mitandao ya kijamii akisema ameagiza kuondolewa sokoni soseji hizo, huku
akiwashauri wananchi kuacha kula.
Motsoaledi alisema ingawa kiwanda cha RCL hakijatajwa kama
chanzo cha ugonjwa huo, kitengo chake kinafanyiwa uchunguzi.
Ugonjwa wa listeriosis uliibuka Desemba mwaka jana na
umeshasababisha vifo vya watu 180.
Comments