Jamii kote nchini imeombwa kuwasaidia wasiojiweza katika msimu huu wa sikukuu ili wasiojiweza nao wajihisi kama ni sehemu ya jamii hiyo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Erick inayotoa elimu na Marekebisho kwa Wenye Ulemavu (EMFERD) Josephine Bakhita , Wilayani Mvomero mkoani Morogoro.
Mama Josephine Bakhita akiwa na watoto wenye ulemavu wa viongo na akili. Watoto hao ni wa familia moja ya Mzee Semgweno, wanaoishi katika kijiji Cha Mvomero, Kata na Tafara ya Mvomero, Wilani Mvomero mkoni Morogoro. Mama Josephine Bakhita kupitia Taasisi yake ya EMFERD amekuwa akisaidia familia hiyo kupata mahitaji mbali mbali japo uwezo wa taasisi ya EMFERD haukidhi mahitaji ya familia hiyo na walemavu wengine wanaolelewa na taasisi hiyo.
Bakhita alisema kuwa jamii za walemavu, yatima, wazee na watoto wanaoishi katika mazingira magumu ni vema zikawa zinakumbukwa misimu ya sikuu kwani nao wanahitaji kufurahi pamoja na wana jamii wengine.
“ Wapo watoto wenye ulemavu wa viungo na akili, wapo watoto yatima, wapo wafungwa, wagonjwa wapo wazee, wapo wafungwa katika kipindi hiki cha Pasaka ni muhimu sana jamii hizi zikakumbukwa ili nazo zisijihizi kutengwa na wanajamii wenzao” Alisema Bakhita.
Aliongeza kusema kuwa baadhi ya familia zinakula vizuri na kuvaa vizuri, zipo familia ambazo zinasaza vyakula na hata kutupa jalalani ama kutumia vileo, basi ni vema kwa taasisi, mashirika na watu binafsi kuyafikiria makundi ambayo yamepoteza matumaini na hayana uwezo wa kupata hata mlo mmoja kwa kuwapatia chochote kitu iwe ni mavazi au vyakula kwa lengo la kuzifanya jamii hizo kufurahi na kutohisi kutengwa.
“ Msimu huu wa sikuu ya Pasaka, wakristu wanakumbuka kuteswa, kufa na kufufuka kwa Yesu. Ni kipindi muafaka kwa jamii zetu kurudisha matumaini yaliyokufa ya watu waliokata tamaa kwa kushiriki pamoja nao ili kuwapa faraja na kuifufua mioyo ya watu hao.” Aliongeza kusema Mama Josephine Bhakita.
Naye Mlezi wa Familia ya watoto wanne wa familia moja wenye ulemavu wa viungo na akili,Elizabeth Semgweno, alisema kuwa, familia zenye watoto wenye ulemavu wa akili na viungo zinakumbana na changamoto kubwa ya malezi ya watoto hao na wanaiomba jamii kutochoka kuwasaidia.
“Kulea watoto wanne wa familia moja wenye ulemavu wa viungo na akili ni mtihani mkubwa sana. Zipo changamoto nyingi tunazokumbana nazo, chakula, maradhi na mavazi ni miongoni mwao. Tunaiomba jamii itusaidie walau kipindi hiki cha sikukuu ili nasi pamoja na watoto wetu tupate faraja na kujihisi kuwa jamii ipo pamoja nasi”. Alisema Eliza.
Na Mwandishi wa EMFERD
Comments