SIMBA haitaki mchezo linapokuja suala la mechi za kimataifa. Baada ya kutambua ina mtihani mgumu, imefanya jambo la maana ikiiwahi mapema Al Masry ya Misri itakaoumana nao wikiendi hii katika mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho.
Kwanza Simba imeamua kubadilisha mfumo wao wa uchezaji watakapoenda kucheza na Wamisri, pia wakaamu kumtanguliza kigogo wao, Musley Ruwey nchini humo ili kuweka mambo sawa na kudhibiti hila zozote za wapinzani wao.
Simba imepanga kuondoka kesho Jumatano, baada ya mipango yao ya kuondoka jana Jumatatu kukwama, lakini hilo limelisaidia benchi la ufundi kupiga akili ya ziada na kubadilisha mfumo wa uchezaji kwa vijana wao.
Benchi hilo lililopo chini ya Kocha Pierre Lechantre limeanza mazoezi ya mfumo mpya wa kupata ushindi ugenini baada ya sare ya mabao 2-2 nyumbani katika mechi ya kwanza ya michuano hiyo ya CAF iliyopigwa Jumatano iliyopita jijini Dar.
Kocha Msaidizi wa Simba, Masudi Djuma alisema hawataenda kuutumia mfumo waliouzoea kwa muda mrefu wa 3-5-2 na badala yake watatumia mifumo miwili kamambe ya kuwazima mapema Waarabu hao kutoka Mji wa Port Said.
“Tutacheza mfumo wa 4-5-1 au 4-4-2, ili kuwa na wachezaji wengi katika kuzuia lakini hata kushambulia.
“Tutakuwa makini na kupunguza makosa ambayo tulifanya kwenye mechi ya kwanza,” alisema Djuma.
Wakati Djuma akisema hayo, bosi wake Mfaransa Lechantre alitamba kama Al Masry waliweza kupata mabao mawili katika mechi ya ugenini, hata wao wana uwezo huo kwani mpira unaochezwa ni ule ule.
“Kweli Al Masry wana timu nzuri na wachezaji wazuri, ila hata Simba nayo ni hivyo hivyo, kwa maandalizi tuliyoyafanya tuna imani yatakuwa na msaada kwetu katika mechi ya marudiano tunaoutambua utakuwa mgumu kwetu,” alisema Lechantre.
MAPEMA TU
Kutokana na umuhimu wa mchezo huo, Simba itakwenda nchini Misri keshokutwa Jumatano ili kuzoea mazingira mapema kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa Jumamosi hii.
Habari mbaya ni, pamoja na Simba kuwahi nchini humo, rekodi zinaonyesha haijawahi kupata ushindi wowote katika ardhi ya Waarabu ndani ya dakika 90.
Simba imewahi kucheza na timu za Ismailia, Al Ahly na Zamalek za Misri na kupoteza michezo hiyo, japo ilifaidika kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Zamalek mwaka 2003 na kusonga mbele kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumzia rekodi hiyo mbovu, Djuma alisema timu yao sasa imebadilika na wanaweza kuvunja mwiko huo.
“Kuhusu Simba kutokuwa na rekodi nzuri kutoka katika timu za Kiarabu au ukanda huo hilo lilikuwa miaka ya nyuma na hii ni timu tofauti.
“Simba hii ni mpya kwani Al Masry wana makosa mengi ambayo waliyafanya katika mechi ya mwanzo lakini hata tulivyowaangalia katika video tumeyaona makosa na tunaweza kuyatumia na tukapata matokeo ya kusonga mbele,” alisema.
“Rekodi ipo kwa ajili ya kuvunjwa, hivyo kutokuwa na rekodi nzuri bado tunaweza kuivunja ingawa si jambo rahisi kwani wapinzani nao wana timu nzuri, ila tunaenda kupambana tupate matokeo ya ushindi kwao kwani inawezekana,” alisema.
- Get link
- X
- Other Apps
- Get link
- X
- Other Apps
Comments