Polisi nchini Rwanda imetangaza kuwatia kizuizini wachungaji 6 na viongozi wa makanisa kutoka baadhi ya makanisa yaliyofungwa kwa amri ya serikali ya nchi hiyo.
Wiki iliyopita serikali ya nchi hiyo iliamrisha kufungwa kwa makanisa zaidi ya 700 kwa madai ya kutotimiza kanuni za ujenzi wa makanisa yao.
Miongoni mwa waliokamatwa ni kasisi Askofu Innocent Rugagi, kiongozi wa kanisa la "Abacunguwe" ambaye ni mojawapo ya wachungaji mashuhuri nchini Rwanda.
Polisi inawashutumu kwa kufanya mikutano ya siri kukaidi uamuzi wa serikali.
Ni hivi karibuni serikali iliyapiga marufuku makanisa zaidi ya 700 kwa kukosa miundo mbinu msingi na yalituhumiwa kusababisha kelele nyingi .
Askofu Rugagi alisikika akishutumu kile alichokitaja kuwa uamuzi wa ghafla kuyafunga makanisa bila ya ilani ya kutosha.
Wachungaji hao wamekamatwa baada ya rais Paul Kagame wiki iliyopita kushutumu wazi kile analichokitaja kuwani idadi kubwa ya makanisa haramu nchini.
Kiongozi huyo aliuliza iwapo makanisa hayo, kwa maneno yake, yana manufaa yoyote kuwepo.
Ameendelea kusema kuwa yanasababisha tishio kwa usalama.
Jumla ya makanisa 700 yamefungwa, mengi yakiwa ni makanisa madogo madogo yaliyoanzishwa hivi karibuni.
Kulingana na bodi ya taifa hilo inayohusika na uongozi, makanisa yanatakiwa kufwata taratibu za ujenzi wenye miundo msingi stahiki na shahada ya elimu ya theolojia kwa wachungaji.
Rwanda inajadili sheria mpya ambayo itahusu mashirika yenye misingi ya imani na dini yanayo endeshwa na wahubiri kuwa wahubiri hao lazima wawe na shahada za elimu ya theolojia.
Kwa sasa polisi wanasema bado wanafanya uchunguzi wa kina. Source http://www.bbc.com
Comments