Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga sasa inahitaji ushindi wa mabao 2-0 ugenini, ili kusonga mbele kwa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Bao la mshambuliaji Obrey Chirwa halikutosha kuisaidia Yanga kuepuka kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya 2-1 na Township Rollers kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizunguzia kipigo hicho Kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa alisema kosa kubwa walilofanya ni kuwaruhusu wapinzani wao kuchezea sana mpira.
"Tumeshajua wapi ambapo tumekosea baada ya mchezo huu, tuliwaacha sana wenzetu wakicheza, kikubwa tunajipanga kwaajili ya mechi ijayo," alisema.
Yanga inayoandamwa na majeruhi katika kikosi chake cha kwanza ilianza mchezo huo wakimtumia kipa wake chipukizi Ramadhani Kabwili huku mkongwe Mcameroon Youth Rostan akiwa benchi.
Kocha wa Yanga, George Lwandamina ambaye jana hakuonekana katika mkutano wa wanahabari aliingia katika mchezo huo akitumia mfumo wa 4-4-2, kwa kuwaanzisha mbele Chirwa na Ibrahim Ajibu.
Lwandamina anayehusishwa na kutakiwa na Zesco alionekana kuzidiwa mbinu na mpinzani wake Nikola Kavazovic wa Rollers ambaye alisema tangu juzi kwamba ataingia uwanjani kwa kuhakikisha hawapi Yanga nafasi kumiliki mpira.
Mbinu hiyo ya Msebria zilifanikiwa baada wachezaji wa Rollers kutawala mchezo wao kuamua ni vipi mchezo utakwenda huku Yanga wakionekana muda mwingi wakipoteza malengo yao.
Dakika 11, Township Rollers ilipata bao la kuongoza lililofungwa na Lemponye Tshreletso kwa shuti kali akiwa umbali mita 25.
Baada ya bao hilo Yanga iliamka na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika 30, wakati Chirwa alipomalizia kazi nzuri ya Papy Tshishimbi aliyegongeana na Pius Buswita kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha Pili Yanga iliingia kwa kasi na kufanya mashambulizi mfululizo langoni mwa Township lakini kukosa umakini kwa washambuliaji wake Ajibu, Chirwa, Juma Mahadhi kuliwanyima mabao.
Kila dakika zilivyokuwa zinaenda ndivyo wachezaji wa Yanga walivyoanza kuonyesha dalili za kuchoka na kutoa mwanya kwa wageni kutawala mchezo.
Mabingwa hao wa Botswana aliandika bao la pili dakika 83, kupitia Motsholetsi Sikele akipiga shuti mbele ya kipa Kabwili.
Kabla ya bao hilo Rollers walipigiana pasi zaidi ya 20 wakiwavuta wachezaji wa Yanga kabla ya kupenyezwa pasi kwa mfungaji akiwa ndani ya eneo la 18 la Yanga.
Kocha mkuu wa Township Rollers, Kavazovic alisema bado anaiheshimu Yanga licha ya kupata ushindi huo.
"Nimekuwa nikiifuatilia klabu hii wiki tatu nyuma ili nijue wanachezaje, wazuri bado nawaheshimu katika mchezo wa marudiano tukiwa nyumbani," alisema Kavazovic.
Huu ni ushindi wa kwanza kwa Township Rollers kushinda ugenini katika mashindano ya CAF tangu 2015.
Kabla ya mechi hiyo mabingwa hao wa Botswana mafanikio yao makubwa ugenini ni kupata sare moja tu, lakini michezo yote wamefungwa ila ni hatari zaidi wanapocheza nyumbani.
Rollers imefungwa mechi moja tu nyumbani ilipofungwa na Kaizer Chiefs bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Februari 28, 2015 katika mchezo wa kwanza waliocheza Afrika Kusini pia Chiefs ilishinda 2-1.
Tangu wakati huo imecheza mechi sita za mashindano na kirafiki na klabu mbalimbali imefungwa michezo mitatu ya ugenini na kupata sare moja wakati ikishinda mbili za nyumbani.
Comments