Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu imewaachia huru kwa dhamana viongozi sita wa Chadema pasipo viongozi hao kuwepo mahakamani
Hata hivyo watatakiwa kuripoti kituo cha polisi Kila siku ya Alhamisi.
Akitoa uamuzi wake, Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri amewataka washtakiwa hao kuwa na wadhamini wawili kila mmoja na kusaini kwa maandishi dhamana ya Sh milioni 20."Kila mshtakiwa atasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 20, wadhamini pia watasaini kiwango hicho, washtakiwa wakiwa nje kwa dhamana wanatakiwa kuripoti polisi mara moja kwa wiki, ambayo ni kila siku ya Alhamisi," amesema Hakimu Mashauri.
Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa ni miongoni mwa wanachana na viongozi wa juu wa Chadema waliofika kufuatilia mwenendo wa kesi inayowakabili Mbowe na viongozi wengine wa chama.
Wafuasi wa chama hicho pia walijitokeza wakiwa nje ya mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam wakisubiri uamuzi wa mahakama juu ya rufaa .
Viongozi hao walikamatwa Jumanne wiki hii na kufikishwa mahakamani ambapo wanakabiliwa na makosa manane ikiwa pamoa na uchochezi na kukusanyika katika mkutano wa hadhara pasipo na kibali.
Awali wakili wa serikali Faraja Nchimbi alisema kosa lao la kwanza ni kuandaa mikusanyiko ama maandamano yasiyo na uhalali.
Miongoni mwa mashtaka waliyosomewa ni pamoja na maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa chuo cha NIT Akwilina Akwiline.
Wanashtakiwa pia kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali wilayani Kinondoni shtaka linalowakabili washtakiwa wote.
Washtakiwa wote walikana mashtaka yote dhidi yao ambapo Wakili Nchimbi alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na aliomba tarehe kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.
Awali kupitia afisa habari wa Tumaini Makene, Chama hicho kililaani vikali kukamatwa kwa viongozi wao na kusema ''Zimekua ni sarakasi dhidi ya upinzani...njama hizi dhidi viongozi wetu hatutaweza kuzinyamazia, tutaendelea kuzilaani na tunaangalia uwezekano wa kuchukua hatua za kisheria''.Source BBC.
Comments