WANANCHI wa Kata ya Pugu, Mtaa wa Mustafa, wamempongeza Mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita kwa kuwapelekea maji safi na salama huku wakibainishiwa kuwa ameweka historia ya kutatua changamoto hiyo.
Kata hiyo ambayo inadaiwa kuongoza kwa changamoto ya maji kwa kipindi kirefu, imejenga historia leo kupitia kwa Meya Mwita ambaye amepeleka maji na hivyo wananchi hao kuondokana na adha hiyo iliyodumu kwa kipindi kirefu.
Meya Mwita ameahidi pia kuongeza huduma hiyo kwenye maeneo ambayo yanachangamoto ya maji.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mtaa huo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mustafa Bahati Lusizi alimshukuru Meya Mwita kwa juhudi alizozionyesha hadi kufanikisha kuwapatia huduma hiyo kwani kilikuwa ni kilio cha muda mrefu.
Amesema tangu kuingia kwa uongozi wake umekuwa wa mafanikio makubwa na kwamba waliomba kwa kipindi kifupi kupatiwa maji huduma hiyo na hivyo wameweza kutekelezewa kwa wakati walioahidiwa.
Alifafanua kuwa kwa sasa wananchi wa eneo hilo wanapata maji safi na salama, nakuomba kufikishiwa kwa huduma hiyo maeneo mengine yenye changamoto hizo.
“ Kwaniaba ya wananchi wa mtaa huu, tunakupongeza Meya umefanya kazi kubwa, eneo hili linachangamoto ya maji, lakini kwa sasa itakuwa historia ,kwenye huu utawala wako tutakukumbuka kwa kutuondolea kero hii” amesema Lusizi.
Awali Meya Mwita akizungumza na madiwani, wananchi walioshuhudia mradi huo wa maji, amesema kuwa juhudi zilizofanyika katika eneo hilo, zitatumika kwenye maeneo mengine ili kila mwananchi wa kata hiyo aweze kunufaina na kuondokana na kero hiyo.
Meya Mwita amewaelekeza viongozi hao akiwemo Diwani wa Kata hiyo Boniventure Mphuru hadi kufikia Aprili Mwaka huu, wananchi hao wapate huduma hiyo ya maji kwa bei ya shilingi 50 kwa kila ndoo badala ya sh.100 ambayo wanauziwa kwa sasa.
“ Nia yangu katika nafasi niliyonayo ni kuhakikisha kwamba kero mbalimbali zinazo wakabili wananchi ninazitatua, Kata ya Pugu inachangamoto sana ya Maji, lakini sasa ninawaambia itakuwa historia kwenye uongozi wangu” amesema Meya Mwita.
Wakati huo huo, Meya Mwita ameridhishwa na ujenzi wa ukuta wa Dampo la Pugu Kinyamwezi unaoendelea hivi sasa ambapo wakandarasi wanaojenga ukuta huo wamemtoa wasiwasi wa kieleza kuwa ujenzi huo hautakuwa na madhara kwa wananchi waliopo karibu na eneo hilo.
Aidha mbali na ujenzi huo wa ukuta, lakini pia ameridhishwa na utekelezaji wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha zege yenye urefu wa kilomita 0.7 kuingia kwenye Dampo hilo ambapo utawezesha barabara hiyo kupitika kwa kipindi chote cha mwaka bila tatizo lolote.
Comments