Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma kuburuzwa mahakamani
mwezi Aprili kwa makosa 16 yakiwemo ya kutumia vibaya ofisi wakati akiwa
madarakani na ufisadi.
Duru za habari nchini Afrika Kusini likiwemo gazeti la News24
limeeleza kuwa Zuma atafikishwa kizimbani katika Mahakama Kuu mjini
Durban tarehe 6 Aprili 2018 kwa makosa 16.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na msemaji wa bodi ya kuzuia na
kupambana na rushwa nchini humo, Brigedia Hangwani Mulaudzi amesema kuwa
mwishoni mwa wiki hii watawasilisha barua kwa mawakili wa Zuma juu ya
wito huo.
Mulaudzi amesema kuwa Zuma atakabiliwa na mashtaka makubwa 16 ambapo
rushwa na Matumizi mabaya ya ofisi yanatajwa kuwa ni moja ya mashtaka
yaliyopewa kipaumbele.
Imeelezwa kuwa Jacob Zuma alifanya malipo ya risiti 783 kiholela,
kwenye ununuzi wa silaha na vifaa vya jeshi nchini Afrika Kusini ambapo
inakadiriwa kuwa ametumia mabilioni ya fedha kwenye ununuzi huo.
Mwaka 2012, Zuma aliingia kwenye kashfa nzito baada ya kutengeneza
nyumba yake ya kifahari kwa kutumia fedha za serikali, ambapo alitumia
zaidi ya dola milioni 25 za kimarekani.
Hata hivyo, kashfa hiyo ilitetewa na baadhi ya wabunge wa chama
tawala nchini humo ANC, ambapo walieleza kuwa ukarabati huo ulizingatia
vigezo.
Mnamo Februari 14, 2018. Mzee Zuma alitangaza kung’atuka madarakani
baada ya shinikizo kubwa kutoka kwa wanachama wa ANC na nafasi yake
kuchukuliwa na aliyekuwa Makamu wake wa Rais, Cyril Ramaphosa.
Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya kisiasa barani Afrika wanasema
kuwa hatua ya Zuma kufunguliwa mashtaka ni mpango wa chama cha ANC
kujisafisha, ili kujiwekea nafasi ya kushinda uchaguzi mkuu ujao wa
urais mwakani.
Chanzo:Gazeti la News24
Comments