Josephine Matiro amefunga mafunzo ya siku tatu yaliyofanyika katika manispaa ya Shinyangayalihudhuriwa na wanawake na vijana 60 kutoka vikundi 20
Katika kufunga mafunzo ya siku tatu yaliyofanyika katika manispaa ya Shinyanga, Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amefunga mafunzo hayo kwa vikundi vya wajasiriamali vya wanawake na vijana manispaa ya Shinyanga yaliyolenga kuwajengea uwezo wa namna ya kutumia vizuri fedha za mikopo walizopewa na manispaa hiyo.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na wanawake na vijana 60 kutoka vikundi 20 vya wajasiriamali ambao wamepata mikopo ya shilingi milioni 125.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo jana Jumatatu Machi 19, 2018 Matiro aliwataka vijana na wanawake hao kutumia fedha walizopewa kwa malengo waliyokusudia na kuhakikisha wanaanzisha viwanda vidogo vitakavyoinua uchumi wao.
“Tumieni mikopo hii kwa ajili ya kuanzisha viwanda vidogo ili kumuunga mkono rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli anayetaka Tanzania iwe nchi ya viwanda, pale mnapokwama tafadhali wasilianeni na viongozi wa serikali,tutawasaidia na pia tutatembelea miradi yenu ili tujue mnachofanya”,alisema Matiro.
Aidha aliwataka vijana na wanawake kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo kwenye halmashauri za wilaya ,mikopo ambayo haina masharti magumu wala riba kubwa ukilinganisha na taasisi za kifedha (benki).
“Msikubali kukata tama kwamba maisha ni magumu,hata siku moja serikali haiwezi kugawa pesa kwa mtu mmoja mmoja,anzisheni vikundi vya ujasiriamali,kisha ombeni mikopo kwenye halmashauri,pesa zipo”,aliongeza Matiro.
Kwa upande wake kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga Octavina Kiwone alisema vikundi hivyo vimepata mkopo wa shilingi milioni 125 kutoka mfuko wa wanawake na vijana ikiwa ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya manispaa hiyo.
“Katika mwaka wa fedha 2017/18 manispaa imelenga kutoa shilingi milioni 208 kwa ajili ya vijana na wanawake,katika awamu hii ya kwanza tumetoa shilingi milioni 125 kwa vikundi 11 vya wanawake na 9 vya vijana”
“Baada ya kutoa mikopo hiyo,tumeona ni vyema tuwape elimu ya kuhusu namna ya kunufaika na mikopo,mafunzo yamedumu kwa muda wa siku tatu,na kipaumbele cha manispaa ni kuviwezesha vikundi vya wanawake na vijana kuanzisha viwanda vidogo vidogo”,aliongeza Kiwone.
Naye Afisa Maendeleo ya vijana Manispaa ya Shinyanga,Charles Luchagula alisema manispaa hiyo inaendelea kupokea maombi ya mikopo kwa vijana na wanawake ili kujiinua kiuchumi na kujikimu kimaisha.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo walisema kupitia mafunzo hayo ya siku tatu wamepata elimu kuhusu namna ya kuanzisha biashara na kutafuta masoko,kutengeneza mnyororo wa thamani kutunza kumbukumbu na vifungashio na umuhimu wa uwekaji lebo.
Walisema pia wamejifunza taratibu za utoaji wa mikopo na urejeshaji wa mikopo,wajibu wa kiongozi wa kikundi,ukweli kuhusu Ukimwi,ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na elimu kuhusu mfuko wa bima ya afya (CHF) iliyoboreshwa.
Comments