Paul Pogba ameibua matumaini mapya juu ya kiwango chake baada ya kufunga bao la ‘maajabu’ wakati timu yake ya taifa ya Ufaransa ikiitandika Urusi 3-1 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa.
Pogba amekuwa na msimu mbaya chini ya kocha Jose Mourinho huko Old Trafford, lakini bao lake tamu la free-kick lililowasili dakika ya nne baada ya mapumziko likaibua hisia kali.
Baba wa kiungo huyo wa Manchester United – Fassou Antoine, aliyefariki mwezi Mei mwaka jana, angetimiza miaka 80 Jumanne usiku na ndipo Pogba akatumia mechi hiyo kama kitu maalum kwaajili ya siku ya kuzaliwa baba yake.
Baada ya kufunga bao lake akashangilia na kufunua jezi yake ili kuruhusu maandishi aliyoyaandika kwenye fulana yake ya ndani yasomeke.
Fulana hiyo iliandikwa ‘Bon Anniversaire, Papa. Allah y Rahmou,’ kwa tafrisi nyepesi yakimaanisha ‘heri ya siku ya kuzaliwa baba, Allah (Mungu) akurehemu’.
Kylian Mbappe aliipa Ufaransa bao la kuongoza dakika ya 41 baada ya kazi nzuri ya Pogba na ukingoni mwa mchezo mshambuliaji huyo wa PSG akaifungia tena nchi yake bao la tatu kunako dakika ya 83. Bao pekee la Urusi liliwekwa wavuni na Fyodor Smolov katika mwa kipindi cha pili.
Comments