MTANDAO wa Jinsia nchini (TGNP Mtandao) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mafunzo ya jinsia(GTI) wameandaa programu maalum ya kuwalea na kuwakuza na vijana wa kike ili kuweza kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
Daktari wa kwanza mwanamke nchi Tanzania Ester Mwaikambo akizindua progaram hiyo mapema leo makao makuu ya Mtandao wa Jinsia(TGNP) yaliyopo mabibo jijini Dar es salaam. |
Programu hiyo iliyopewa jina la “Mentorship Program” itawasaidia watoto wa kike kuweza kusimama wenyewe katika nafasi za uongozi na maamuzi kwa kupewa elimu na watu waliowatangulia katika nafasi hizo au kwa jina lingine makungwi watakao walea na kuwaonyesha njia na mbinu za kuwa kama wao.
Akiongea na waandishi wa habari katika uzinduzi wa programu hiyo leo jijini Dar es salaam Mratibu wa Mafunzo ya Jinsia Jane Tesha alisema kuwa lengo kuu la programu hiyo ni kuwalea vijana wakike walio katika uongozi au wanaotarajiwa kuingia katika uongozi ili waweze kuwa imara katika nafasi zao.
Aliongeza kwa kusema kuwa jumla ya washiriki 33 watapata nafasi ya kukuzwa na kufunzwa jinsi ya kuzitumia rasilimali walizonazo kupitia makungwi walioteuliwa kuwafunza katika nyanja tofauti tofauti.
Aidha Dada Jeni aliendelea kusema kuwa mafunzo hayo yatakuwa ya miezi 6 na washiriki watapewa mafunzo katika Nyanja kama afya, uandisi, wanasheria, biashara na nyingine nyingi ili kuendelea kuongeza pato la taifa kupitia vijana ambao ni asilimia 61 ya watanzania wote.
“Elimu hii tutakayoitoa kwa wanawake hasa vijana ambao ni asilimia 61 ya watanzania wote, itawasaidia kujitambua na kutambua fursa mbalimbali walizonazo na kuwa na ujasiri wa kugombea pamoja na kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi na maamuzi ili kuweza kufikia malengo ambayo 50 kwa 50 katika uongozi kati ya wanawake na wanaume”. Alisema Dada Jeni
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao Lilian Liundi alisema huu ni mwanzo tu tumeanza na vijana wa mjini kwa kuwapa fursa hii lakini tunaandaa mpango mwingine ambao utakuja hivi karibuni ambao utawagusa na wale wa vijijini.
“Kwa wasichana ambao wapo vijijini na hawana chanzo chochote cha mtandao hawa ndio malengo yetu makuu, hivyo basi tutahakikisha wanapata elimu hii kwa kuwapelekea makungwi waweze kuwapika kupitia vituo vyetu vya taarifa na maarifa ili wasiweze kupitwa na programu hii”. Alisema Mkurugenzi
Comments