Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
“Kwa masikitiko nimepokea taarifa ya kifo cha Mwenyekiti Mstaafu
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma Dkt. Walid Amani Kaburu
kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 07 Machi, 2018 katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Dkt. Walid Amani Kaburu atakumbukwa kwa mchango wake alipokuwa
kiongozi katika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM, na alipokuwa Mbunge wa Kigoma
Mjini na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Natoa pole kwa familia yake, wana CCM wote, wananchi wa Kigoma,
ndugu jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu”
Hii ni sehemu ya salamu za rambirambi alizotuma Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Mkuu wa Mkoa wa
Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga kufuatia kifo cha Dkt. Walid
Amani Kaburu.
Pamoja na salamu hizo Mhe. Rais Magufuli ameiombea familia ya
Marehemu na wote walioguswa na msiba huu kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na
ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi na amemuombea Marehemu apumzike
mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
07 Machi, 2018
Comments