Siku ya Ijumaa, Julai 13, 2012 majira
ya saa 4:27 asubuhi gari lenye namba za usajili T 875 AKS aina ya
Toyota Landcruiser, liliwasili katika maegesho ya wizara ya mambo ya
ndani na kisha akashuka Godbles Lema, Dkt. Willibrod Slaa pamoja na
wakili wao Dkt. Rugemereza Nshala, kwa pamoja wakawa wanaelekea mlango
wa kuingilia ndani ya jengo hilo.
Kabla
ya kuingia ndani waandishi walitaka kujua sababu za Dkt. Slaa pamoja na
Lema kufika makao makuu ya jeshi la polisi ambapo walisema walienda
kuitikia wito.
“Tumepata wito na tumeitikia
tambueni mjumbe hauawi sasa ni wito wa namna gani ngoja tukawasikilize
lakini na ninyi waandishi wa habari hampitwi na kitu kila sehemu mpo,”
alisema Dkt. Slaa huku akicheka.
Baada ya kufika mapokezi, Dkt.
Slaa na Lema walielekezwa kwenda chumba namba 703 ambapo walikaa kwa
muda wa dakika tano na kisha wakatoka kuelekea chumba namba 808 huku
ofisa wa Polisi aliyevaa kiraia akiwataka waandishi wa habari
wasiwafuate.
Katika Chumba namba 808
walichoingia ofisa huyo wa Polisi aliwakaribisha huku akisikia
kuwaambia Dkt. Slaa, Lema pamoja na wakili wao Dkt. Nshala kuwa
wakaribie ingawa eneo hilo lipo katika ukarabati na kisha kufunga
mlango.
Akiongea na waandishi wa
habari, msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alisema Dkt. Slaa na
wenzake waliitwa kwa ajili ya maelezo ya awali ya kusaidia uchunguzi
dhidi ya malalamiko yao ya kuuawa.
Alisema Jeshi la Polisi
limefungua jalada la uchunguzi na kwamba mlalamikaji ni ni lazima atoe
maelezo yatakayoweza kufanyika kwa uchunguzi huo kabala ya jalada
kupelekwa kwa Mwendesha Mashitaka, “Tumewaita kwa hati maalum, dhidi ya
malalamiko yao. Naamini tutashirikiana nao kubaini ukweli na kisha
tutafanyia kazi kwa kuwa wajibu wetu ni kumlinda kila mmoja hata kama
atakuwa ametolea malalamiko yake chumbani.” alisema Senso.
Comments