Na Othman Khamis Ame
Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na Wazazi wanahitajika
kuendelea kujenga Misingi ya Maadili imara ambayo inaonekana kulega lega
hasa kwa Vijana kunakosababishwa na Mambo tofauti likiwemo la kukua kwa
Mawasiliano ya Sayansi na Teknolojia Duniani.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati
akiiungua Ijitimai ya 17 ya Kimataifa inayofanyika katika majengo ya
Jumuiya ya Fiy Sabilillah Tablih Markaz Fuoni Migombani nje kidogo ya
Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema Watanzania
wengi hasa Vijana wamekuwa wakijijengea Utamaduni wa kuiga maadili
mabovu badala ya kufanya mema ambayo yanakwenda kinyume na Mila, Silka
na hata Taratibu za Dini.
Balozi Seif alitoa rai kuwa
pamoja na mada nyengine zilizoandaliwa katika Ijitimai hiyo ni vyema kwa
wahadhiri watakaopata fursa waitumie hadhara hiyo kujadili kwa kina
mbinu zitakazosaidia kurejesha maadili mema miongoni mwa Vijana Nchini.
Makamu waPili wa Rais wa
Zanzibar alitahadharisha kwamba mmong’onyoko wa maadili ni tishio kwa
Ustawi wa Taifa lolote lile hapa Duniani.
“Siku hizi si jambo la ajabu
kukutana na kundi la Vijana wa Kiislamu wanatumia dawa za kulevya
zinazopelekea kujiingiza katika vitendo viovu”. Alitanabahisha Balozi
Seif .
Akikumbusha suala la umuhimu wa
Waislamu kufanya kazi, Balozi Seif alisema hakuta kuwa na njia ya mkato
wa kuendesha afamilia bila ya kufanya kazi kwa bidii.
Alisema Uislamu kupitia Kitabu
kitukufu Qurani sdambamba na Hadithi zake imesisitiza umuhimu wa
kufanya kazi za halali ili kuwa na sababu ya kujipatia chumo la halali.
Balozi Seif alikariri moja ya
Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume
Muhammad { SAW } ikisema chumo bora ni lile mja alichumalo kwa mikono
yake.
“ Tabia iliyojengeka katika
Jamii yetu ya ubadhirifu wa Mali za Umma tukumbushane kuwa tabia hiyo
haifai na tuachane nayo mara moja”. Alitahadharisha Balozi Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia waumini wa dini zote Nchini
kwamba Serikali itaendelea kuheshimu uhuru wa kuabudu kwa kushirikiana
na Taasisi zote za Kidini Nchini kwa lengo la kustawisha Jamii yote.
Alisema Katiba ya Nchi ijnaeleza wazi kwamba kila mtu ana haki ya kuabudu dini aitakayo mradi havunji sheria za Nchi.
Kuhusu suala la Sensa ya Watu na
Makazi ya Mwaka 2012 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba
Viongozi wa Dini zote kuhamasisha wafuasi wao kushiriki kikamilifu
katika zoezi la kuhesabiwa linalotarajiwa kufanyia usiku wa kuamkia
tarehe 26 Agisti Mwaka huu.
Comments