Mechi hiyo, ambayo awali ilikuwa ichezwe kesho kwenye Uwanja wa Amaan, sasa itachezwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Taifa.
Katibu
wa kamati ya maandalizi ya michuano hiyo, Suleiman Jabir aliwaambia
waandishi wa habari mjini Dar es Salaam leo kuwa, uamuzi huo umefikiwa
kutokana na timu hizo mbili kugoma kucheza uwanja wa Amaan.
Jabir
amewaomba radhi mashabiki wa soka wa Zanzibar kutokana na fainali hiyo
kuhamishiwa Dar kwa madai kuwa, jambo hilo lipo nje ya uwezo wao.
Awali,
Simba na Azam ziligoma kucheza fainali hiyo kwenye Uwanja wa Amaan kwa
madai kuwa ni mbovu na umesababisha kuumia kwa baadhi ya wachezaji wao.
Makamu
Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' aliwaambia waandishi wa
habari kuwa, eneo la kuchezea soka kwenye uwanja huo ni bovu.
Kaburu alisema wapo tayari kucheza fainali hiyo kwenye uwanja wowote, lakini si Uwanja wa Amaani.
Alisema waliwasilisha malalamiko hayo kwa waandaaji kwa muda mrefu, lakini hawakuweza kuyafanyia kazi.
Kaburu
alisema kutokana na timu yake kushiriki kwenye michuano ya Kombe la
Kagame, wana hofu wachezaji wao wanaweza kuumia zaidi kwenye mechi hiyo.
Aliwataja wachezaji wa Simba walioumia tangu kuanza kwa michuano hiyo kuwa ni Lino Masimbo, Salim Kinje na Mussa Mudde.
Meneja
wa Azam, Patrick Setter alisema klabu yake inawapenda na kuwaheshimu
mashabiki wa Zanzibar, lakini kutokana na hali ya uwanja wa Amaan,
hawawezi kucheza mechi ya fainali visiwani humo.
“Tupo
tayari hata kwenda kucheza Pemba ama kwingine kokote, lakini sio hapa
Amaan. Hofu yetu ni wachezaji wetu wengi zaidi kuumia,"alisema.
Kwa
mujibu wa Patrick, wachezaji wa Azam walioumia tangu kuanza kwa
michuano hiyo ni Michael Kipre, Jabir Azizi na Kipre Tchetche.
Alisema hawagomi kucheza mechi hiyo Uwanja wa Amaan kwa sababu ya maslahi, bali wanajali zaidi afya za wachezaji wao.
Rais wa ZFA, Amani Makungu alisema wapo tayari kupokea lawama kutoka kwa wapenzi wa soka wa Zanzibar, lakini hawana la kufanya.
Alisema
walikuwa wakifikiria kuihamishia mechi hiyo Uwanja wa Gombani, Pemba
lakini wameshindwa kutokana na gharama kubwa kwa vile viongozi wa Simba
na Azam wametaka kusafirishwa kwa ndege.
Inatoka kwa mdau.
Comments