Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa Serikali itahakikisha kambi za wakimbizi wa Burundi katika
Tanzania zinafungwa na wakimbizi wanarudi kwao kwa sababu hawana tena
sababu ya kuendelea kuwa wakimbizi katika Tanzania.
Amesema kuwa hali ya usalama, amani na utulivu katika Burundi ni mazingira mwafaka kwa kila Mrundi kuishi kwao badala ya kuendelea kuwa mkimbizi katika Tanzania.
Rais Kikwete ameyasema hayo, Alhamisi, Julai 19, 2012, wakati alipokutana na kuzungumza na Sheikh Mohammed Rukara, Mjumbe Maalum wa Rais wa Burundi, Mheshimiwa Pierre Nkurunziza, Ikulu, mjini Dar es salaam. Sheikh Rukara pia ni Mkuu wa Uchunguzi wa Malalamiko ya Wananchi (Ombudsman) katika Burundi.
“Tutashughulika na wakimbizi kwa sababu hawana tena sababu ya kubakia Tanzania kama wakimbizi. Tutahakikisha kuwa kambi za wakimbizi wa Burundi katika Tanzania zinafungwa,” Rais Kikwete amemwambia Sheikh Rukara.
Rais pia ameisifu Burundi kwa mafanikio makubwa ambayo yamepatikana tokea amani irejee katika nchi hiyo jirani na hasa tokea Rais Nkurunziza alipoingia madarakani miaka saba iliyopita.
“Mmefanya kazi kubwa na nzuri sana katika ujenzi wa barabara, ujenzi wa shule, ujenzi wa vyuo vya elimu ya juu na zaidi ya yote ujenzi wa amani na umoja. Ni vyema kuwa macho na kuendelea kulinda amani,” amesema Rais.
Sheikh Rukara amemshukuru tena Rais Kikwete kwa mchango wake mkubwa katika kutafuta amani ya Burundi. “Mheshimiwa Rais ulituokoa sana,” amesema Sheikh Rukara.
Miongoni mwa mambo mengine, katika salamu zake maalum, Rais Nkurunziza amemshukuru Rais Kikwete kwa kuhudhuria Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Burundi zilizofanyika mjini Bujumbura Julai 2, mwaka huu, 2012.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Julai, 2012
Comments