JIBU: Asante, nashukuru sana.
SWALI: Kabla ya uchaguzi huu, ulikuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya usajili ya Yanga na sasa ni mjumbe wa kamati ya utendaji. Nini mikakati yako kwa Yanga?
JIBU: Kwa kweli namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa na afya njema hadi sasa. Pia napenda kuwashukuru wanachama wenzangu wa Yanga kwa kuniamini na kunipa kura nyingi kuliko wagombea wote.
Unajua bila ya wanachama kukuamini, hawawezi kukupa heshima kubwa kiasi hiki. Nawaomba waendelee kuniamini na mimi nawaahidi kwamba, nitaitumikia klabu yetu kwa moyo wangu wote na nguvu zote.
Jambo la msingi ni kwamba, viongozi wapya wa Yanga tunakabiliwa na changamoto kubwa ya kuchapa kazi ili kuhakikisha tunaleta mabadiliko makubwa kiuongozi na katika timu ili tuweze kufikia malengo tutakayojipangia. Tunapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia kauli mbiu yetu ya Yanga mbele, nyuma mwiko.
SWALI: Umepanga kufanya nini katika kutekeleza ahadi ulizozitoa kwa wanachama wakati wa kampeni?
JIBU: Nimepanga kufanya mambo makubwa matatu. La kwanza ni kushirikiana na viongozi wenzangu kuhimiza umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama ili kuondoa makundi yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi, ambayo yakiachwa, yanaweza kuwa chanzo cha mgogoro.
Unajua umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama ni jambo muhimu kuzingatiwa kama kweli tunataka kupata maendeleo. Tukigawanyika, hatutaweza kufanikiwa kwa lolote lile. Kwa maana hiyo, nitahakikisha kila mwanachama, kuanzia ngazi ya matawi, anashiriki kikamilifu katika kutoa maamuzi mbalimbali muhimu yanayoihusu Yanga.
Jambo la pili ni kwamba, nitahakikisha Yanga inakuwa na timu imara za vijana wa umri mbalimbali kwa ajili ya kujenga timu bora ya baadaye. Na utaratibu huu utaanzia mikoani kupitia kwa matawi yetu.
Kama utakumbuka vizuri, zamani Yanga ilikuwa ikiyatumia matawi yake ya mikoani kusaka vipaji vya wachezaji. Tumepanga kuurejesha upya utaratibu huu kwa kusaka vipaji vya vijana watakaounda timu hizi za vijana kutoka mikoani na Dar es Salaam. Wachezaji tutakaowachukua ni wale wenye mapenzi ya kweli na Yanga.
Jambo la tatu ni kwamba, nataka kuiona Yanga ikipata mafanikio makubwa katika michuano ya ligi na kimataifa kwa kutoa kipaumbele kwa wachezaji na benchi la ufundi.
Nimepanga kutoa kipaumbele kwa wachezaji na benchi la ufundi kwa sababu kama hawapati haki zao vizuri na kwa wakati, hawawezi kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Hivyo nitahakikisha kuwa, uongozi mpya wa Yanga unawapatia wachezaji haki zao kwa wakati na kwa kiwango kinachokubalika.
Jambo lingine muhimu nitakalolipa kipaumbele ni kuhakikisha kuwa, katiba ya Yanga inafanyiwa marekebisho ili iweze kwenda na wakati na kuondosha kabisa migogoro iliyokuwepo miaka ya nyuma. Ninapenda kuona viongozi wakitimiza wajibu wao bila kuingiliana ama kuwekewa vikwazo na wanachama.
SWALI: Katika msimu uliopita, ulifanikiwa kumsajili mshambuliaji Haruna Niyonzima kutoka APR ya Rwanda kwa pesa nyingi. Na msimu huu pia umechangia usajili wa wachezaji kadhaa wapya. Je, bado una mikakati yoyote ya kusajili mchezaji mwingine mpya?
JIBU: Kwa kawaida huwa napenda sana kufanya kazi zangu kwa siri bila mtu mwingine kufahamu lolote kama ilivyokuwa kwa Niyonzima. Hivyo ni kweli kwamba ninaye mchezaji mwingine ninayeendelea kufanya mipango ya kumsajili na mipango itakapokuwa tayari, tutawajulisha.
SWALI: Kuna taarifa kwamba ulikuwa katika mipango ya kumsajili mshambuliaji Meddie Kagere wa Polisi ya Rwanda na alikuwepo hapa nchini kwa ajili ya mazungumzo na viongozi. Je, mipango hiyo imefikia wapi?
JIBU: Ni kweli tulikuwa na mipango hiyo na niliifanya kwa kushirikiana na wadau wengine wa Yanga, lakini ilikwama kidogo kutokana na kujitokeza kwa hali ya kutokuelewana kati yetu na mchezaji huyo.
Lakini bado hatujakata tama kwa sababu lolote linaweza kutokea kwa vile muda wa usajili bado haujamalizika. Kama utakumbuka, mwisho wa usajili wa wachezaji wapya ni Agosti 10 mwaka huu ifikapo saa 5.59 usiku.
SWALI: Kwa sasa, Yanga inashiriki katika michuano ya Kombe la Kagame mkiwa mabingwa watetezi. Nini mikakati yenu kwa ajili ya michuano hiyo?
JIBU: Japokuwa tulianza vibaya kwa kufungwa na Atletico ya Burundi, mikakati yetu ni kuhakikisha tunautetea vyema ubingwa wetu. Waswahili wana msemo usemao kuteleza si kuanguka. Nawaomba wanachama na mashabiki wa Yanga wawe wavumilivu kwa sababu uwezo wa kufanya vizuri tunao.
Vilevile napenda kuwahakikishia wana Yanga wote kuwa, wasiwe na wasiwasi kuhusu michuano ya ligi kuu kwa sababu timu ipo imara na itakuwa chini ya viongozi makini, hivyo uwezo wa kurejesha taji letu msimu ujao tunao. Kilichotokea msimu uliopita ni matatizo tu madogo madogo, ambayo hayawezi kutokea tena.
Comments