Ndugu zangu,
Afrika yetu ina mambo. ” Ex Africa simper aliquid novi”. Maana yake: “Kila kukicha kitazuka kioja kingine Afrika. Alipata kutamka Ptolemy, mwanafalsafa wa Kiyunani.
Rais wa Liberia Ellen Johnsson yuko nchini mwetu kwa ziara ya Kiserikali. Ujio wake unanikumbusha kila nilichokisoma kuhusu Rais wa Liberia
aliyeitwa William Tubmann, huyu alitawala Liberia kutoka mwaka 1944
hadi 1964. Enzi hizo, alikuwa ni Rais ‘ Mzee wa Makamo’ kwenye ‘Nchi kijana’- Liberia.
Rais Tubmann
alikuwa na vituko haswa. Moja ya vituko vyake ni pale alipokwenda kwa
mara ya kwanza nchini Ethiopia kushiriki mkutano wa Umoja wa Mataifa ya
Afrika (OAU).
Rais Tubmann
alikuwa ni mwoga sana wa kupanda ndege. Basi, akafunga safari ya meli
kutoka Monrovia, Liberia kwenda Ethiopia. Safari ilimchukua mwezi
mzima. Akatua Ethiopia akiwa amechoka na kuwakuta Marais wenzake wa
Afrika wanamsubiri.
Na akawa kivutio kikubwa pia kwa wanahabari. Lakini, Rais Tubmann
aliwaogopa sana wanahabari na maswali yao. Yasemekana katika Urais wake
hakuwahi kujibu swali lolote gumu la mwanahabari.
Pale
Ethiopia, akarushiwa swali kuhusu hali ya siasa nchini mwake. Rais
akaliogopa swali na alikuwa na mbinu zake za kuyakwepa maswali.
Akiulizwa swali huchukua kiko chake na kuanza kuvuta. Na kinachotokea?
Kama
pale Addis Ababa enzi hizo. Rais akalisikia swali, akachukua kiko chake
huku wanahabari wakisubiri kwa hamu kubwa kusikia jibu la Rais. Naye
akiwa amekaa kwenye kiti chake hotelini akavuta ‘ugolo’ wake kwenye
kiko chake.
Kabla hajajibu swali, mara akaanza
kupiga chafya mfululizo. Akapiga chafya weee, mpaka machozi yakaanza
kumtoka. Kila mmoja akamwonea huruma. Na wengine wakaangua vicheko.
Wasaidizi wa Rais wakawataka radhi wanahabari kumruhusu Mheshimiwa Rais akapumzike.
Rais Tubmann akawa ametoka mahali hapo bila kujibu swali hata moja!
Maggid Mjengwa,
Örebro, Sweden
Comments