Waandishi Wetu
NCHI imetikiswa. Mgomo wa walimu ulioanza jana katika sehemu mbalimbali nchini, umeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya elimu huku kukiwa na taarifa za matukio yasiyokuwa ya kawaida yaliyoambatana na mgomo huo usio na ukomo.
Katika sehemu mbalimbali nchini, walimu waliripotiwa kugoma kwa kutoingia madarasani na wengine walifika kazini na kusaini vitabu vya mahudhurio kisha kuondoka hali iliyosababisha wanafunzi kurandaranda ovyo katika sehemu za miji iliyo karibu na shule hizo.
Mjini Dodoma ,wabunge jana walimbana Naibu Spika, Job Ndugai wakitaka shughuli za Bunge zisitishwe ili kujadili mgomo wa walimu ambao umeanza rasmi jana nchi nzima, na kuziacha shule nyingi zikiwa na walimu wakuu na wakuu wa shule pekee.
Hata hivyo, Ndugai alisema Bunge lisingeweza kujadili suala hilo kwani tayari Serikali ilikuwa imelifikisha mahakamani baada ya kushindwa kuafikiana na walimu katika ngazi ya usuluhishi.Wakati hayo yakiendelea, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa amesema Serikali itafuta mishahara kwa walimu walioitikia mwito Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wa kushiriki mgomo ambao alisema siyo halali.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Dk Kawambwa pia aliwaonya walimu ambao alisema wamekuwa wakiwabughudhi wenzao ambao waliamua kwenda kazini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo akiwa Mjini Morogoro aliwaagiza wakuu wa shule za msingi na sekondari mkoani humo kuandaa orodha ya majina ya walimu wasiofika kazini Julai 30 na waifikishe kwa maofisa elimu wa wilaya kabla ya saa 2:00 asubuhi ya Julai 31.
Waandishi wetu katika sehemu mbalimbali nchini pia waliripoti kwamba katika baadhi ya shule, wanafunzi waliruhusiwa kurejea nyumbani mapema kwa maelezo kwamba hakukuwa na masomo.
Hali hiyo ilizua kizaazaa kwani katika baadhi ya mikoa wanafunzi walicharuka na kuitisha maandamano hadi katika ofisi za maofisa elimu wa wilaya, wakitaka Serikali iingilie kati mgomo huo ili waendelee kusoma.
Kadhalika, baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali walinukuliwa wakitoa matamko ya kuwasihi au kuwaamuru walimu warejee madarasani, kauli ambazo hata hivyo, hazikubadili uamuzi wa walimu hao.
Wanafunzi waandamana
Maandamano ya wanafunzi yaliripotiwa katika Mji wa Tunduma, Mbeya ambako polisi walitumia mabomu ya machozi kuwadhibiti wanafunzi.
Wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi katika Wilaya ya Mbozi mkoani humo waliandamana wakidai haki ya kufundishwa. Hata hivyo, maandamano hayo yaliingiliwa na vibaka ambao baadaye walivunja ofisi za Halmashauri ya Mji wa Tunduma na kuiba mali kadhaa kisha kuchoma nyaraka zilizokuwemo.
Tukio hilo lilitokea asubuhi wakati wanafunzi wa shule 14 za msingi zilizopo katika halmashauri ya Tunduma walipojikusanya na kufanya maandamano hadi nyumbani kwa diwani na baada ya kumkosa walielekea kituo cha polisi na baadaye ofisi katika hizo.
Comments