Na Othman Khamis Ame
Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inakusudia kujenga misingi imara ya kukuza ubia baina ya Sekta
ya Umma na ile Binafsi ili kuwajengea uwezo Wazanzibari kushiriki
kikamilifu katika shughuli za Kiuchumi Nchini.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud
Mohamed ameeleza hayo wakati akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato
na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa Mwaka wa
fedha wa 2012/2013 katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea
kwenye ukumbi wa Baraza hilo hapo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mh. Aboud alisema misingi hiyo {
Public –Private Partnership } itakwenda sambamba na Sekta Binafsi
kuwekeza kwenye Miradi mbali mbali ya Maendeleo ya Kiuchumi na Utoaji wa
Huduma.
Waziri Aboud alifahamisha kwamba
Sekta Binafsi ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa Uchumi wa Taifa, hivyo
kupitia uwekezaji wa Sekta hiyo Nchi itakuwa na fursa kubwa ya kuongeza
Pato la Taifa pamoja na ajira kwa Vijana.
Mh. Aboud alieleza kwamba katika
kuweka mazingira mazuri ya kukuza fursa za uwekezaji, Serikali kwa
kushirikiana na Wahisani tofauti itaimarisha zaidi miundo mbinu ili
kutanua wigo wa eneo hilo muhimu.
Aliitaja miundo mbinu hiyo kuwa
ni pamoja na Umeme, Bara bara, Bandari ikiwemo ujenzi wa njia ya pili ya
Umeme kutoka Ubungo Dar es salaam hadi Mtoni Unguja.
Comments