ASHANGAA SMZ KUZIDIWA NGUVU, UAMSHO YAKUBALI KUSHIRIKI MCHAKATO WA KATIBA MPYA
Mwadhama Polykarp Kardinal Pengo
|
Ibrahim Yamola
ASKOFU
Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo
ameitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ‘kudhibiti wahuni
wanaotaka kuvuruga amani visiwani humo’.
Kauli hiyo ya Pengo ni ya kwanza
tangu kuibuka kwa vurugu visiwani Zanzibar mapema mwezi huu, na
kusababisha uharibifu wa mali, huku makanisa yakilengwa zaidi na kikundi
kinachojiita cha Jumuiya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (JUMIKI).
Pengo alitoa kauli hiyo wakati
wa ibada maalumu iliyofanyika katika Kanisa la Msalabani Bagamoyo,
mkoani Pwani, ikiwa ni maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Shirika la Roho
Mtakatifu, utakaofanyika kwa siku 30 kuanzia jana.
Kardinali Pengo alisema, ‘wahuni
hawawezi kuizidi Serikali makini’.“Makanisa yetu yamecomwa moto na watu
wahuni. Kama Serikali ipo na haiwezi kuchukua hatua dhidi ya wahuni,
usalama uko wapi?” alihoji Kardinali Pengo.
“Wahuni wanaweza kutuunguzia
makanisa saba kwa mpigo, lakini mbele ya hapo kuna makanisa kadhaa
ambayo yalikwishaunguzwa na kubomolewa na hao wahuni,” alisema.Pengo
aliendelea kuhoji, “Kama sasa wahuni wameishinda nguvu Serikali ya watu
kwa hiyo tutawaliwe na wahuni na wafanye lile wanalolitaka, tunajiuliza
tunakwenda wapi?
Mara baada ya vurugu za
Zanzibar, jopo la maaskofu kutoka madhehebu mbalimbali, walifanya
mazungumzo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), huku wakiituhumu
kushindwa kudhibiti vitendo vya uchomaji moto makanisa na kuihadharisha
kuchukua hatua za haraka.
Jana, Pengo alilitaka shirika
hilo kumsaidia Askofu Augustine Shayo wa Jimbo Katoliki Zanzibar,
kuunganisha nguvu zao katika harakati za kuimarisha amani.
Comments