Mamia
ya wafuasi wa Udugu wa Kiislamu wamekusanyika katika uwanja wa
al-Tahrir mjini Cairo kusheherekea baada ya chama hicho kutangaza
ushindi katika uchaguzi wa rais.
Chama cha Udugu wa Kiislamu
kimeripoti kwenye tovuti yake kwamba mgombea wake Mohamed Mursi
amejipatia asilimia 52 katika uchaguzi huo uliofanyika kwa siku mbili
mwishoni mwa juma baada ya asilimia 95 ya kura kuhesabiwa kutoka vituo
vya kupiga kura.
Mursi, profesa wa uhandisi,
alisimama dhidi ya Ahmed Shafiq, kamanda wa zamani wa kikosi cha anga,
ambaye alitumika kwa muda mfupi kama waziri mkuu wakati wa utawala wa
Mubarak.
Katika hotuba aliyoitowa kwa
njia ya televisheni mapema leo hii, Mursi amesisitiza ahadi yake ya
kujenga taifa la Misri la kisasa chini ya misingi ya kiraia, na amesema
kwamba hatotaka kulipiza kisasi au kujaribu kuwaandama wapinzani wake.
Ameuambia mkutano wa waandishi wa habari ulioonyeshwa kwenye televisheni
kwamba atakuwa rais kwa Wamisri wote - Waislamu na Wakristo.
Mursi, ambaye anaongoza chama
cha Udugu wa Kiislam cha Uhuru na Haki, ametowa wito kwa Wamisri
kuungana kuwa kitu kimoja ili kujenga mustakbali mzuri utakaokuwa na
uhuru, demokrasia, maendeleo na amani. Amesema ujumbe wake ni wa amani
kwa kila mtu duniani.
Comments