MAWAKILI wa Serikali jana waliwasilisha vielelezo Mahakama kuu kuthibitisha kwamba umri wa msanii wa filamu Elizabert Michael ni zaidi ya miaka 18.Habari zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na mawakili wawili; mmoja wa Lulu na mwingine wa Serikali ambao hawakutaka kutajwa, zimeeleza kuwa vielelezo hivyo vimewasilishwa jana mahakamani hapo.
Habari zimeeleza kuwa moja ya vielelezo
hivyo vya Jamhuri ni Mkanda wa video aina ya CD, yenye mahohjiano kati
ya mshtakiwa huyo na mtangazaji mmoja nchini.
"Vingine ni maelezo ya mshtakiwa huyo aliyoyatoa polisi wakati alipohojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili, maombi ya hati ya kusafiria (Passport) na maombi ya leseni ya udereva, alisema mmoja wa mawakili hao.
Awali vielelezo hivyo walitakiwa kuviwasilishwa juzi, lakini ilishindikana na badala yake vikawasilishwa jana.
Baada ya vielelezo kesi hiyo itasikilizwa Juni 25 mwaka huu. Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kumuua msanii mwenzake, Marehemu Steven Kanumba aliyefariki dunia nyumbani kwake Sinza, April 7, 2012.
Hata hivyo umri wake umezua utata baada ya mawakili wake wanaomtetea kudai kuwa bado ni mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama hati ya mashtaka inavyoonyesha.
Hivyo mawakili hao walilazimika kuwasilisha maombi mahakamani kuiomba mahakama iruhusu ufanyike uchunguzi wa umri sahihi wa mshtakiwa huyo na ikiridhika kuwa ni mtoto basi kesi yake iendeshwe kwa misingi ya kesi za watoto wanaokinzana na sheria ili kulinda maslahi yake.
Juni 11, 2012 Mahakama Kuu ilikubali yenyewe kufanya uchunguzi huo kwa lengo la kubaini usahihi wa umri wa mshtakiwa huyo na ikaziagiza na kuzipangia tarehe pande zote katika kesi hiyo kuwasilisha mahakamani hapo vielelezo watakavyovitumia katika hoja zao.
Jopo la mawakili wanaomtetea Lulu likiongozwa na Kennedy Fungamtama Juni 13 waliwasilisha mahakamani hati za viapo vya wazazi wake na vielelezo vingine kikiwemo cheti cha kuzaliwa na cha ubatizo vinavyoonesha kuwa bado ni mtoto.
Lakini taarifa zilizopatikana mahakamani hapo zinaeleza kuwa vielelezo vilivyowasilishwa na Jamhuri vinaonesha kuwa mshtakiwa huyo ni mtu mzima kwa kuwa kwa mujibu wa vielezo hivyo ana umri zaidi ya miaka 18.
Viapo vya wazazi wa mshtakiwa huyo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Peter Kibatala ambaye ni mmoja wa mawakili wanaomtetea Lulu vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo ana umri wa miaka 17.
Viapo hivyo ambavyo Gazeti hili limefanikiwa kuviona ni kiapo cha mama yake Lulu Lucresia Augustin Kalugila, mkazi wa Dar eS Salaam na kiapo cha baba mzazi Michael Kimemeta, mkazi wa Moshi.
Viapo vyote vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo alizaliwa April 16, 1995 katika kituo cha Afya Muhimbili na kupewa cheti cha kuzaliwa namba B.0318479 cha Julai 23, 2004.
Pia viapo hivyo vinaeleza kuwa baada ya kuzaliwa mshtakiwa, mama yake alimpa jina la Diana Michael Kimemeta, lakini alimpeleka mtoto huyo Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ndugu zake, walimpa jina la Elizabeth, jina la bibi yake Elizabeth Shikana.Source: Ujana Tz Blog
Comments