Waziri wa Uchukuzi Dr.Harrison Mwakyembe. |
Mussa Juma, Dodoma
BAADA
ya kusafiri kwa treni kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, Waziri wa
Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amebaini hujuma nzito katika Shirika la
Reli Tanzania (TRL) ikiwamo ofisa mmoja kuwaibia abiria kwa kughushi
viwango vya nauli na ameagiza afukuzwe kazi.
Licha
ya kuagiza kutimuliwa kwa ofisa huyo, pia alitangaza kuandaliwa
utaratibu wa kufanya mabadiliko kadhaa katika kuboresha usafiri huo,
ikiwamo kuondoa malipo ya nusu nauli kwa watoto wadogo kuanzia miaka
mitatu hadi miaka 10 na pia kuondolewa kwa utaratibu wa malipo ya
mizigo midogo ya abiria.
Juzi,
Dk Mwakyembe ambaye tayari amewang’oa vigogo wanne wa Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL), aliamua kusafiri kwa treni hadi Dodoma akitokea Dar es
Salaam ili kujionea utendaji kazi wa shirika hilo.
Mara
baada ya kuwasili katika Stesheni ya Dodoma saa 1:30 asubuhi, Waziri
Mwakyembe alizungumza na waandishi wa habari na kusema akiwa katika
safari hiyo, amepata fursa za kutembelea mabehewa yote na kuzungumza na
abiria.
Dk
Mwayembe alisema ingawa safari ilikuwa nzuri, kuna mengi ambayo
ameyabaini ambayo ni pamoja na abiria kulipa nauli kubwa na kuandikiwa
tiketi tofauti jambo ambalo alisema ni wizi na kamwe wizara yake
haiwezi kulifumbia macho.
“Unakuta
nauli halali ni Sh9,000 lakini, abiria ameandikiwa Sh29,000. Sasa
nimeagiza huyu anayehusika afuatiliwe na kujulikana na nipewe taarifa
ameondolewa,” aliagiza Dk Mwakyembe.
Alisema
pia katika safari hiyo, alibaini uchakavu mkubwa wa mabehewa na hakuna
tofauti ya daraja la tatu na la kwanza, upungufu mwingine ni katika
utendaji na taratibu jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa hatua.
Dk
Mwakyembe alisema si vyema mtoto kuanzia miaka mitatu kulipishwa nusu
nauli, kwani taratibu zinapaswa kufanywa ili hadi mtoto wa miaka 10
ikiwezekana asilipishwe nauli kwani treni ndiyo usafiri wa umma.
Kuhusu
mizigo, alisema kwa sasa mizigo ya abiria inalipiwa kwa kilo kama
ilivyo usafiri wa ndege jambo ambalo si sawa kwani mzigo wa abiria
kuanzia kilo 20 unalipishwa jambo ambalo linapaswa kuangaliwa.
“Usafiri
huu mimi nasema ndiyo wa umma hivyo, tusizuie watu kupeleka hata zawadi
nyumbani kwao ni vyema tuwe na utaratibu walau mizigo kidogo ya abiria
isilipiwe,” alisema Dk Mwakyembe.
Chanzo Mwananchi. http://www.mwananchi.co.tz/biashara
Comments