Na Joachim Mushi, Thehabari.com- Mafinga
WANAFUNZI wenye ulemavu anuai katika Shule ya Msingi Makalala wameiomba
Serikali na wadau wengine kuwasaidia kuwajengea mazingira bora ya
kujifunzia kwa watoto wenye ulemavu ili waweze kupata elimu bora kama
ilivyo kwa watoto wengine.
Kauli hiyo imetolewa katika risala ya wanafunzi hao iliyosomwa jana
Wilayani Mafinga kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika iliyofanyika
kiwilaya kwenye Shule ya Msingi Makalala nje kidogo ya Mjini wa Mafinga.
Katika maelezo yao watoto hao wameiomba Serikali na wadau wengine
kuwatizama kundi la watoto wenye ulemavu anuai kwa jicho la karibu, hasa
katika uboreshaji wa mazingira jumuishi ya kujifunzia katika shule zenye
watoto wenye ulemavu.
Pamoja na hayo wanafunzi hao walemavu wameomba kuboreshewa mazingira ya
lijifunzia katika Shule yao ya Makalala, ikiwa ni pamoja na kuwajengea
chumba maalumu kwa ajili ya kujifunzia kitakachokidhi mahitaji ya kundi
hilo maalumu.
Akizungumza katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Mafinga, Bi. Farida Mwasumilwe alisema licha ya Serikali
kujitahidi kuboresha huduma mbalimbali kwa watu wenye ulemavu bado kuna
changamoto nyingi hivyo kuomba wadau kushirikiana kwa pamoja kuwasaidia
watu wenye ulemavu hasa watoto.
Bi. Mwasumilwe aliwataka wadau mbalimbali kusaidiana kutoa elimu kwa baadhi
ya wazazi ambao bado wamekuwa na kasumba ya kuwaficha watoto wenye ulemavu
ndani hivyo kukosa haki za msingi ikiwemo elimu, ambayo ndio mkombozi pekee
kwa kundi hilo.
"Naomba tusaidiane kuwafichua watoto wote walemavu ambao baadhi ya wazazi
wamekuwa wakiwaficha ndani hivyo kukosa haki yao ya msingi. Pia jamii haina
budi kusaidia malezi ya watoto kwani mzigo huu sio waserikali pekee,"
alisema Mwasumilwe ambaye ni Ofisa wa Elimu Shule za Msingi Wilaya ya
Mafinga.
Katika maadhimisho hayo yalioambatana na michezo mbalimbali kwa makundi ya
watu
wenye ulemavu, Shirika la Sightsavers limeahidi kumalizia ujenzi darasa
la kisasa pamoja na baadhi ya vifaa vya kujifunzia litakalokuwa na
uwezo wa kufundishia wanafunzi wenye ulemavu shuleni hapo.
Shirika
hilo mbali na kukabidhi fimbo 35 maalumu za kutembelea kwa wanafunzi
wasioona pia limeahidi kutoa gari la kisasa kwa shule ya Makalala ili
kuwasaidia wanafunzi walemavu hasa wasioona kupata huduma zao nje ya
kituo hicho pale inapohitajika. (kila fimbo moja ina thamani ya sh
50,000 za kitanzania).
Maadhimisho
hayo yaliandaliwa na taasisi anuai zinazofanya kazi na watu wenye
ulemavu, zikiwemo Chama cha wasioona Tanzania (TLB), Kituo cha Habari
Kuhusu Walemavu nchini (ICD), Sightsavers, CCBRT, INUKA, SHIVYAWATA kwa
kushirikiana na Serikali ya Tanzania. Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku
ya Mtoto wa Afrika mwaka huu inasema, "Haki za Watoto wenye Ulemavu; Ni
Jukumu letu Kuzilinda, Kuziheshimu, Kuziendeleza na Kuzitimiza".
*Habari
hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa
kushirikiana na Kituo cha Habari Kuhusu Walemavu Tanzania (ICD)
Comments