KAZI YAKE KUTAFUTA VYANZO VIPYA VYA MAPATO, KUONGEZA BAJETI YA MAENDELEO
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda |
Neville Meena na Mussa Juma, Dodoma
WAZIRI
Mkuu, Mizengo Pinda ameunda Kamati Maalum ya mawaziri sita kusaidia
mchakato wa marekebisho ya Bajeti ya Serikali ambayo mjadala wake
utahitimishwa kesho.Kuundwa kwa kamati hiyo kunazifanya kamati
zinazoifanyia kazi Bajeti ya 2012/2013 kufikia tatu.
Ijumaa iliyopita wabunge wa CCM
waliunda kamati ndogo kwa ajili ya kusaidi pamoja na mambo mengine
kuangalia vyanzo vingine vya mapato na kuona iwapo bajeti ya maendeleo
inaweza kuongezwa, kukidhi kiu ya wabunge.
Kamati nyingine ni ile ya Fedha
na Uchumi ya Bunge ambayo tayari imetoa maoni yake bungeni kuhusu
Bajeti, lakini ikabainisha kuwapo kwa kasoro kadhaa ambazo zinapaswa
kurekebishwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alikiri kuundwa kwa kamati
hiyo, lakini akakataa kutoa taarifa za kina kuhusu suala hilo kwa
maelezo kwamba huo ni utendaji wa kawaida wa shughuli za Serikali.
“Sidhani kama hiyo ni habari
kubwa ya kwenda kwenye public (kwa umma). Kwanza siyo kamati ya
mawaziri, haiwezi kuwa hivyo, na huo ni utendaji wa kawaida wa ndani ya
Serikali maana sisi tuna mambo mengi tunafanya,”alisema Lukuvi na
kuongeza:
“Kamati za utekelezaji wa
shughuli za Serikali ziko nyingi sana na siyo tu za Bajeti. Kwa hiyo
ndio maana nakwambia hilo ni jambo dogo sana ambalo mimi sidhani kama
linahitaji kutangazwa, kama lingekuwa hivyo mimi ningekuwa wa kwanza
kutaka kulizungumzia,” alisema.
Comments