Neville Meena na Mussa Juma, Arumeru
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kilianza kutumia helkopta
katika kampeni zake za kumnadi mgombea wake wa ubunge katika uchaguzi
mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.
Habari
ambazo gazeti hili limezipata zinasema helkopta hiyo itaendelea kutumika
hadi siku ya mwisho ya kampeni na kwamba itakiwezesha chama hicho
kufanya mikutano kati ya mitano hadi minane kwa siku.
Mkuu wa
Operesheni wa uchaguzi wa Chadema katika jimbo hilo, John Mrema alisema
kuanza kutumika kwa helkopta hiyo kutamwezesha mgombea wao kufanya
mikutano mitano kwenye kata tano tofauti.
Mikutano ya
jana ilifanyika katika vijiji vya Ngurdoto Kata ya Maji ya Chai, Ngabobo
Kata ya Ngarenanyuki, Kijiji cha Sakila Kata ya Kikatiti na vijiji na
kata za King’ori na Nkoanrua.
Helkopta
hiyo ilianza kuonekana katika anga la Usa River, Arumeru jana asubuhi na
hakukuwa na taarifa za awali kuhusu ujio wake kama ambavyo chama hicho
kimekuwa kikifanya katika kampeni nyingine zilizotangulia.
Helkopta
hiyo yenye maneno makubwa CHADEMA, ilitumika wakati wa uzinduzi wa
kampeni za chama hicho zilizofanyika katika Uwanja wa Shule ya msingi
Leganga, Usa River Machi 10 mwaka huu na tangu wakati huo haikuwahi
kuonekana tena hadi jana.
Dk Slaa na ardhi
Katikamikutano
ya jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alimshambulia Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Gudluck Ole Medeye
kwamba anahusika na kukodisha shamba la Valesca lililo Jimbo la Arumeru
Mashariki kwa wawekezaji kwa bei ya kutupa.
Akizungumza
katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Ngabobo, Ngurdoto na Sakila,
Dk Slaa alisema ni aibu mawaziri wa Serikali ya CCM kuomba kura katika
Jimbo la Arumeru Mashariki huku wakiwa ni waasisi wa mpango wa kugawa
ardhi ya umma kwa walowezi wa kizungu.
Alisema
Naibu Waziri huyo, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, kabla
ya kukubali kutolewa shamba hilo lenye zaidi ya ekari 400 ambalo
Serikali itapata kiasi cha Sh2.4 milioni tu kwa mwaka walipaswa
kuwakumbuka wananchi.
“Hivi kweli
nyie wananchi wa Meru hamuhitaji ardhi hii na mngeshindwa kulipa
Sh6000 kwa ekari moja ili muweze kulima, kama alivyouziwa mzungu?
”alihoji Dk Slaa.
Aliwataka
wakazi wa jimbo hilo, kukubali mabadiliko sasa kwa kuchagua mbunge wa
upinzani ili aweze kuhoji ardhi ya Meru ambayo kiasi kikubwa
kimegawanywa kwa walowezi kutoka nje ya nchi.
Vituo bandia
Wakati hayo
yakiendelea, tuhuma kwamba kuna vituo 55 vya bandia vilivyoandaliwa kwa
lengo la kutumika kuiba kura kwenye uchaguzi huo, zinaonekana
kugonganisha vichwa vya maofisa wa uchaguzi.
Tuhuma hizo
ni zile zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa juzi
kwamba kuna vituo 55 bandia 55 vya kupigia kura katika uchaguzi huo
mdogo madai ambayo yalikanushwa na Msimamzi wa Uchaguzi wa Arumeru
Mashariki, Trasias Kagenzi.
Juzi Kagenzi
alipozungumza na waandishi wa habari alisema vituo halali ambavyo
anavitambua ni 327 tu na hakukuwa na kituo ambacho kimeongezwa na kwamba
hata kama ikitokea hivyo, itakuwa ni baada ya majadiliano na vyama
vyote shiriki.
“Vituo
vilivyopo ni 327 pekee, na kama ikitokea kituo kinakuwa na watu zaidi ya
500 ndipo kunaweza kuongezeka, lakini historia inajionesha kila
uchaguzi mdogo unapofanyika idadi ya wapigakura inapungua,”alisema
Kagenzi.
Lakini jana
Kagenzi alikiri kuwapo kwa kasoro kwenye orodha ya vituo hivyo na kwamba
alikuwa anawasiliana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ili kuwezesha
kufanyika kwa marekebisho.
Maeleo ya
Kagenzi yanatokana na ushahidi ambao gazeti hili liliupata kwa kuona
orodha ya vituo hivyo, ambayo ilikuwa ikionyesha takwimu mbili tofauti
za idadi ya vituo vya kupigia kura.
Katika
orodha hiyo, safu ya idadi ya vituo vya kupigia kura katika kata 17 za
jimbo hilo ilikuwa ikionyesha vituo 327, wakati safu ya mwisho ya orodha
hiyo hiyo ilikuwa ikionyesha kuwapo kwa jumla ya vituo 382, likiwa ni
ongezeko la vituo 55.
Waraka wa
orodha hiyo unaonyesha kuwa katika Kata ya Akheri kutakuwa na vituo 20
idadi ambayo inayofautiana na iliyotolewa na tume ambavyo ni vituo 18.
Kata
nyingine ambazo vituo hivyo vinaonekana kuongezwa ni Kikatiti vituo 22
badala ya 18, Kata ya Kikwe vituo 12 badala ya halali 11, Kata ya
Kingori vituo 29 badala ya halali 26 na Kata ya Leguruki vituo 23 badala
ya halali 20.
Kata
nyingine ni Makiba vituo 21 badla ya halali 18, Majiya chai 24 badala ya
29 halali, Maroroni vituo 21 badala ya 17 halali, Mbuguni vituo 25
badala ya halali 21,Nkoarsambu vituo 10 badala ya 8 vinavyohitajika na
Kata ya Ngarenanyuki ambako vimeongezwa vituo sita kutoka halali 20 hadi
26.
Orodha hiyo
ambayo Kagenzi alithibitisha kwamba ilikuwa na makosa pia ina kasoro
katika Kata za Nkoaranga ambako vituo vimeongezwa kutoka halali 17 hadi
22, Pori kutoka vituo halali 16 hadi 20, Nkwandua kutoka vituo 22 hadi
kufikia 25 na Kata ya Seela - Sing’isi vituo hivyo viliongezwa kutoka
halali 12 hadi 15.
Kata
nyingine ni Songoro nyumbani kwa Mgombea wa Chadema, Joshua Nassari
vipo vituo 15 na hakuna kilichoongezeka huku Kata ya Usa River ilikuwa
na vituo 36, lakini vimeongezeka vitano na kufikia 41.
Kagenzi
alisema alipowasiliana na idara ya teknolojia ya habari ya NEC kuhusu
kasoro hizo walimwambia kwamba orodha ya awali haikuwa toleo la mwisho
na kwamba wangefanya marekebisho ya kuondoa kasoro hizo.
“Wameniambia
kwamba hiyo orodha ilikuwa ni working draft tu (rasimu ya kufanyiwa
kazi), kwahiyo nimeomba hiyo orodha kamili ya mwisho, wakishanitumia
nitaisambaza kwa vyama husika,”alisema Kagenzi jana.
Baadaye
msimamizi huyo wa uchaguzi alisema wataalamu kutoka NEC walitarajiwa
kuwasili Arumeru jana mchana kwa ajili ya kurekebisha kasoro hizo pamoja
na kufanya maandalizi mengine kwa ajili ya uchaguzi huo mdogo.
Hata hivyo,
kauli ya Kagenzi ilikuwa ikipishana na ile iliyotolewa na Mkurugenzi wa
Uchaguzi, Julius Mallaba ambaye awali alisema hakukuwa na vituo vya
nyongeza kama ilivyodaiwa na Dk Slaa.Soma zaidi www.mwananchi.co.tz
Comments