Wanafunzi wakiwa wa darasa la Tano na la Sita wakiwa darasani kwa pamoja
WAKATI Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nchini ikijipanga kuanza
kufundisha kwa kutumia teknolojia ya kompyuta katika shule mbalimbali,
wanafunzi wa darasa la tano na sita wa Shule ya Msingi Mengwa bado
wanatumia darasa moja kwa wakati mmoja.
Hali hiyo imejulikana juzi baada ya mwandishi wa habari hizi
kutembelea shule hiyo, iliyopo Kata ya Maneromango, Wilaya ya Kisarawe
mkoani Pwani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mwalimu Mkuu wa Shule ya
Msingi Mengwa, Peter Gadie alisema kitendo cha wanafunzi hao kutumia
darasa moja kimefanya wapunguziwe muda wa vipindi wa kawaida ili
kupishana kwa zamu kutumia darasa hilo.
Alisema badala ya kila kipindi kufundishwa kwa dakika harobaini walimu
wameamua kufundisha kwa dakika ishirini kila kipindi ili kupeana zamu
kuwafundisha wanafunzi hao.
Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia darasa hilo likiwa na wanafunzi wote yaani wa darasa la tano ambao wapo 24, na darasa la sita wakiwa 29 wakiendelea na masomo kwa pamoja huku wakitenganishwa kwa mistari ya madawati.
Akizungumzia staili ya ufundishaji wa walimu kwa kutumia darasa moja,
Gadie alisema mwalimu wa darasa la tano anapoingia darasani huendelea
na kipindi kwa dakika 20 huku akiwataka wanafunzi wa darasa la sita
kujiinamia na kujisomea ama kuendelea na kazi walizoachiwa na mwalimu
aliyetoka punde.
"Anapoingia mwalimu kufundisha darasa moja uwaamuru wanafunzi wa darasa lingine wajisomee
ama kuendelea kufanya kazi ambazo wameachiwa na mwalimu
aliyetoka...kweli wanapata usumbufu lakini haina namna maana
tunaupungufu wa madarasa shuleni kwetu," alisema Gadie akizungumza na
mwandishi wa habari hizi.
Aidha alisema tatizo hilo halipo kwa wanafunzi wa darasa la sita na la
tano pekee, kwani wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili nao usomea
darasa moja kwa kupokezana saa; ambapo darasa la kwanza huingia saa
mbili hadi saa sita na baadaye kuwapisha darasa la pili ambao huingia
saa sita na kuendelea hadi mchana.
Alisema upungufu wa vyumba vya madarasa umeifanya shule hiyo kukodisha
ukumbi wa kuoneshea video kijijini Mengwa na kulifanya darasa la awali
kwa wanafunzi wa shule hiyo wanaosoma darasa la awali kabla ya
kujiunga na darasa la kwanza.
Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
Comments