JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
MABADILIKO KATIKA SEKTA YA MISITU
Ujumbe huu Ulitolewa kwa mara ya kwanza na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Ezekiel Maige kwa Wavunaji wakubwa wa misitu, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na wadau wengine wa misitu
Sao Hill Mafinga tarehe 19 Machi 2012
Ndugu Wadau wa Misitu,
Natumia
fursa hii kuwafahamisha kuwa kuongezeka kwa mahitaji ya mazao ya
misitu, kumesababisha msukumo mkubwa kwa wananchi kutaka kuvuna mazao ya
misitu kutoka kwenye mashamba ya misitu ya serikali. Kutokana na
msukumo huo wa mahitaji ni dhahiri kuwa mabadiliko ya haraka
yanahitajika ili kusimamia ipasavyo uzalishaji, uvunaji na usimamizi wa
bei ya mazao ya misitu. Mabadiliko haya yatafanikishwa na wadau wa mazo
ya misitu, hususan Sekta Binafsi na Wakala wa Misitu Tanzania (Tanzania
Forest Service – TFS).
Katika
miaka mitatu iliyopita, uzalishaji wa mbao umeshuka kutoka mita za
ujazo 1,500,000 hadi 1,200,000. Kufuatia kukua kwa uchumi watu wengi
sasa wanahitaji kujenga nyumba za kisasa, hivyo mahitaji halisi ya mbao
kwenye soko yameongezeka kutoka mita za ujazo 2,000,000 hadi 5,000,000.
Ongezeko hili limetokana pia na kupanuka kwa soko la nje hasa katika nchi za Kenya, Djibouti, Sudan Kusini, Uarabuni na India.
Pamoja na ongezeko hili la soko na kushuka kwa uzalishaji, hadi sasa hakuna
mabadiliko katika jitihada za kuongezeka kwa uzalishaji, wala Serikali
haijanufaika na ongezeko hilo la soko kwa sababu bei imeshuka kwa
asilimia thelathini (30%) kutoka bei ya juu ya mwaka 2007. Hali hii
imesababisha utitiri wa waombaji wa mazao ya misitu na malalamiko mengi
kuhusu ugawaji wa vibali vya uvunaji.
Kwa
hiyo Serikali imeamua kufanya mabadiliko ya muda mfupi ya utaratibu wa
utoaji vibali kwa kuanzisha fomu maalum ambayo itajazwa na waombaji. Hata hivyo, mabadiliko haya ni ya muda tu. Bado mabadiliko makubwa ya muda mrefu yanahitajika.
Maeneo yanayohitajika kufanyiwa mabadiliko ni kama ifuatavyo::-
1.
Kuongeza mapato ya Serikali kwa kurekebisha bei ya tozo za Serikali
angalau zifikie gharama halisi za uzalishaji. Kwa sasa, bei ya kuuzia ni
54% ya gharama halisi ya uzalishaji wa miti ya kutengenezea karatazi
(“pulp”) na asilimia 90 kwa miti ya mbao.
2.
Kuongeza mapato ya Serikali kwa kurekebisha bei ya vibali vya
kusafirishia nje ya nchi (export permits). Hii ni kwa lengo la kuifanya
nchi ifaidike na soko kubwa la nje na kukatisha tamaa ya kuuza mbao nje
ya nchi, hivyo kupunguza bei za mbao hapa nchini.
Aidha,
Wakala wa Hudma za Misitu Tanzania (TFS) umetakiwa kuimarisha ukaguzi
katika mipaka kwa kuanzisha vituo na kupeleka watumishi katika vituo
vyote vya mipakani. Kwa sasa kazi hiyo ya ukaguzi inafanywa na Maafisa
Kodi wa TRA.
3.
Kuweka udhibiti wa bei kwa kuanzisha mfumo wa uzalishaji na usambazaji
wa jumla na rejareja kwa kuanzisha mawakala watakaopatikana kwa tenda
ambao watauza mazao ya misitu kwa bei elekezi itakayowekwa na Serikali.
4.
Kuongeza uzalishaji kwa kuweka mikataba na mawakala ya kuwataka wawe na
mashamba yao katika kipindi cha miaka 15 - 20. Kwa kufanya hivyo baada
ya miaka 20 ijayo, angalau asilimia arobaini (40%) ya malighafi za mbao
itakuwa inatoka kwenye mashamba binafsi. Kwa sasa asilimia tisini na
nane (98%) ya mbao zinatoka kwenye mashamba ya miti na hifadhi za misitu
ya serikali.
Ili
kufikia hatua hii, mikataba iliyopo kati ya Serikali na wawekezaji
itabidi irekebishwe au ivunjwe. Majadiliano kuhusu suala hili,
yanatakiwa yaanze sasa na mikataba mipya iwekwe kati ya sasa na mwaka
2014.
5.
Mapungufu ya kimkataba na kiusimamizi yanayofanya wawekezaji wakubwa
kuuziwa malighafi kwa bei ya chini, huku wavunaji wadogo wakiuziwa
malighafi hizo hizo kwa bei ya juu yatarekebishwa kuanzia msimu ujao,
Julai 2012. Aidha, ili kufikia lengo la kuzalisha karatasi kamili hapa
nchini, ruhusa ya kusafirisha karatasi ambazo hazijafikia kiwango cha
mwisho cha etengenezaji (“semi-processed papers”) itaangaliwa upya.
6.
Ili kuimarisha matumizi ya malighafi kidogo zilizopo, Wakala wa Misitu
Tanzania - TFS unatakiwa kuanza utaratibu wa kugawa malighafi kwa
kutazama matumizi ambapo wavunaji watakuwa wanapewa malighafi kwa
kipindi kifupi, yaani kwa mwezi. Baada ya kuvuna na na kumaliza kutumia, mvunaji ataandaa taarifa itakayoonyesha malighafi hiyo ilivyotumika ndipo aweze kupewa mgao mwingine unaofuata.
Mabadiliko
hayo ni badala ya kupewa mgao wa mwaka mzima ambao wahusika huwa hawana
uwezo wa kuutumia wote, badala yake wanawauzia watu wengine kwa
ulanguzi. Aidha, TFS ianzishe utaratibu wa kugawa malighafi za “chips”
kwa kiwanda cha karatasi cha Mufindi Paper Mill (MPM), badala ya kugawa
malighafi ya miti iliyokomaa kama inavyofanyika hivi sasa.
7.
Ili kuongeza motisha na uzalishaji kwa wananchi waishio jirani na
mashamba ya miti, TFS ianzishe utaratibu wa kuwasaidia walimaji wadogo
wa miti. Kadiri itakavyowezekana, misaada ya ujirani mwema itakayotolewa
na TFS kwa wananchi ilenge katika kuimarisha sekta ya misitu.
Aidha, Mfuko wa Misitu Tanzania (Tanzania Forest Fund - TFF)
uimarishwe kwa kuongezewa vyanzo vya mapato kwa kushirikisha wadau wa
maendeleo. Pia mfuko huo uimarishwe kiutendaji kwa kuwa na menejimenti
yake ambayo itakuwa inatoa mikopo ya muda mrefu na ruzuku kwa wakulima wadogo wa miti.
8.
Ili kuongeza ulinzi kwenye mashamba ya Serikali, Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS) uweke mkakati maalum wa kubainisha mipaka na
kuilinda. Pia, TFS iandae mkakati maalum wa kupanda miti kwa maeneo
yasiyo na miti, ama, kwa kupanda wenyewe au kutumia sekta binafsi kwa
mikataba maalum ya muda mrefu (long term concessations).
Kwa
mfano, Shamba la Miti la Sao Hill linaweza kuingia mikataba ya muda
mrefu na wadau maana ukubwa wa shamba hilo ni hekta 130,000, lakini
zilizopandwa miti hadi sasa ni takriban hekta 50,000 tu.
Yapo
maeneo mengi yanayoweza kuwekewa mikataba ya kupanda miti, kama vile
mashamba ya Serikali ya Buhindi mkoani Mwanza na Rubare mkoani Kagera.
9.
Ili kukabiliana na changamoto ya uvamizi wa maeneo ya hifadhi na
mashamba ya miti, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) uanzishe
dawati maalum la kusimamia migogoro kwa majadiliano na kwa kutumia
taratibu za kisheria.
Imetolewa na
Mhe. Ezekiel M. Maige (Mb)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII.
19 Machi 2012
Comments