Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad Ajionea Uvamizi Unaofanywa Nje ya Uzio Wa Uwanja wa Amaan Zanzibar
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na
baadhi ya watendaji wa Wizara ya Habari, Wizara na Ardhi, na Vikosi vya
SMZ baada ya kukagua uchafuzi wa mazingira katika eneo la uwanja wa
Amaan.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiangalia
uchafuzi wa mazingira nje ya uzio wa uwanja wa Amaan wakati alipofanya
ziara ya kutembelea maeneo yaliyovamiwa. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais na MBM Dr. Mwinyihaji Makame, na katikati (mwenye suti) ni
Waziri wa Maji, Makaazi, Maji na Nishati Mhe. Ali Juma Shamhuna.
Meneja
wa Uwanja wa Amaan Khamis Ali Mzee, akitoa maelezo kuhusiana na
uvamizi wa eneo hilo, wakati Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Maalim Seif Sharif Hamad alipofanya ziara ya kutembelea eneo hilo.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika
ziara ya kutembelea maeneo yaliyovamiwa nje ya uzio wa uwanja wa Amaan.
Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Mhe. Abdallah Mwinyi Khamis na
kushoto ni Meneja wa Uwanja wa Amaan Khamis Ali Mzee.
Baadhi
ya watendaji wa Wizara ya Habari, Wizara na Ardhi, na Vikosi vya SMZ
wakimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif
Hamad baada ya kukagua uchafuzi wa mazingira katika eneo la uwanja wa
Amaan.Picha zote na Salmin Said -Ofisi Ya Makamu wa Kwanza wa Rais Wa
Zanzibar
--
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameutaka
uongozi wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kulipima upya eneo
la uwanja wa Amaan ili likabidhiwe uongozi wa uwanja huo kwa ajili ya
kuliendeleza.
Hatua
hiyo imekuja kufuatia uvamizi unaofanywa nje ya uzio wa eneo hilo
ambao pia husababisha uharibifu wa mazingira kwa kuchimbwa mchanga
pamoja na kutupwa taka kiholela.
Maalim
Seif ametoa agizo hilo baada ya kutembelea maeneo yaliyofanyiwa
uvamizi huo na kutaka hatua za haraka zichukuliwe ili kudhiti uharibifu
usiendelee.
Ameitaka
Wizara hiyo kulipima tena eneo la nje ya uwanja huo lililobakia na
kulimikisha kwa Wizara ya Habari, utamaduni, utalii na michezo, ili
liweze kutumika kwa shughuli za maendeleo kama ilivyokusudiwa ikiwa ni
pamoja na kujenga viwanja vya michezo ya ndani (Indoor games).
Ameusisitiza
uongozi wa uwanja wa Amaan kuliwekea udhibiti eneo hilo mara
wanakapokabidhiwa nyaraka za umiliki, ili kuepusha uvamizi mwengine
usije kujitokeza.
Makamu
wa Kwanza wa Rais pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi kukaa
pamoja na watu wanaojishughulisha na upasuaji wa magogo katika eneo
hilo, ili kusaidia ulinzi wa eneo linalochimbwa mchanga, sambamba na
kuangalia uwezekano wa kubadilisha mfumo wa usafirishaji wa magogo na
bidhaa zitokanazo na magogo hayo kwa kutumia usafiri wa magari badala
ya ule wa magari ya punda na ng’ombe uliozeleka.
Amesema
hatua hiyo itasaidia kudhibiti uchimbaji wa mchanga katika eneo hilo
pamoja na kusimamia marufuku ya uingiaji wa wanyama katika eneo la mji.
Katika
hatua nyengine Maalim Seif ameutaka uongozi wa uwanja wa Amaan kukaa
pamoja na Wizara ya Habari pamoja na ile inayohusiana na vikosi vya SMZ
ili kujadiliana juu ya namna ya kutatua tatizo la ulinzi katika uwanja
huo, baada ya kubainika kutokuweko maelewano mazuri kati ya taasisi
hizo, hali iliyopelekea walinzi wa JKU kuondoka katika eneo hilo.
Awali
meneja wa Uwanja wa Amaan bw. Khamis Ali Mzee amebainisha kuwa walinzi
wa JKU waliondoka baada ya kuwalalamikia kwa kutotekeleza majukumu yao
ipasavyo.
Nae
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) Kanal Sudi Haji Khatib amesema
walilazimika kuwaondosha askari wao katika eneo hilo baada ya kukosa
mashirikiano mazuri kutoka kwa uongozi wa Uwanja wa Amaan.
Waziri
wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mhe. Ali Juma Shamhuna kwa upande
wake ameahidi kulishughulikia suala la upimaji wa eneo hilo ndani ya
kipindi cha mwezi mmoja na kuchukua hatua zinazostahiki.
Meneja
wa Uwanja wa Amaan Bw. Khamis Ali Mzee alidai kuwa sehemu ya eneo
linalolalamikiwa aliwahi kupewa mtu kwa ajili ya kuliendeleza lakini
ameshindwa kufanya hivyo na kusababisha kuwa sehemu ya kutupia taka
(jaa).
Amesema
kwa vile uongozi wa uwanja umeshapata muwekezaji atakayeiendeleza
hoteli ya uwanjani kuwa na hadhi ya “nyota nne hadi tano”, ni vyema
eneo hilo likabidhiwe kwa uongozi wa uwanja huo ili liweze kuwekwa
katika hali nzuri, sambamba na kulinda hadhi ya hoteli hiyo.
Na
Hassan Hamad
Ofisi Ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar
Comments