YUMO PIA KADUMA, WASEMA WANAMTANDAO NI CHANZO CHA UFISADI
Elias Msuya
MAKADA
watatu wakongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Kaduma, Dk Hassy
Kitine na Joseph Butiku, wameibuka na kukitabiri anguko chama hicho
tawala kwa kile walichosema, kwenda kinyume na misingi ya kuasisiwa
kwake.
Kauli za
makada hao maarufu, zinakuja kipindi ambacho upepo wa kisiasa umekuwa
ukivuma vibaya ndani ya chama hicho kikongwe nchini na barani Afrika,
kutokana na vita ya makundi kati ya watuhumiwa wa ufisadi na wale
wanaojipambanua kwamba ni wazalendo na wapinga ufisadi.
Wakizungumza
juzi usiku katika kipindi cha "Je, tutafika?" Kilichorushwa na kituo
cha luninga cha Channel ten, makada hao walitoa kauli hizo nzito huku
wakishambulia kundi la wanamtandao ndani ya chama hicho, vitendo vya
rushwa wakati wa uchaguzi na vitendo vya ufisadi vinavyolitikisa taifa.
Kaduma
Kaduma
ambaye aliwahi kuwa Waziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya
Mwalimu Julius Nyerere, alisema hali ndani ya CCM sasa ni mbaya na
imefika hapo kwa sababu ya kuacha misingi ya TANU iliyoasisiwa na
Mwalimu Nyerere.
“Kwa hali
ilivyo, CCM kinaweza kusambaratika wakati wowote. Sisi tuliingia kwenye
TANU kutokana na misingi ambayo Mwalimu Nyerere aliiweka,” alionya
Kaduma.
Kaduma
aliitaja misingi hiyo kuwa ni pamoja na imani kuwa binadamu wote ni
ndugu, kuwatumikia watu kwa moyo wote, kujitolea nafsi kuondoa
umasikini ujinga na maradhi, rushwa ni adui wa haki hivyo ni kosa kutoa
au kupokea rushwa, kutotumia cheo cha umma kwa maslahi binafsi, kusema
kweli daima na kuacha fitina, kujielimisha kadiri ya uwezo na kutumia
elimu hiyo kwa manufaa ya umma.
Alisisitiza,
“Mwalimu hakuwa akiongea nadharia, ndiyo maana mwaka 1955 aliacha kazi
aliyokuwa nayo ya ualimu iliyokuwa na mshahara mzuri na kwenda
kuimarisha chama cha TANU ilikuwa ni ku-risk (kujiweka kwenye hatari).’’
Dk Kitine
Dk
Kitine akizungumzia barua zilizowahi kuandikwa na Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku kwa wenyeviti wa CCM
(Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete), na kutojibiwa na viongozi hao,
alisema hata angekuwa yeye asingezijibu kwa sababu ndiyo mfumo wa chama
hicho kutotatua na kuficha matatizo.
“Barua ya
Butiku kwenda kwa Mwenyekiti wa zamani na wa sasa haikujibiwa..., hata
ningekuwa mimi nimeandikiwa barua na mambo ninayofanya ni wazi,
nisingeijibu. Mimi siwalaumu. Hiyo ni moja ya matatizo na utamaduni wa
chama tawala kutokuwa na utamaduni wa kutatua matatizo,” alisema Dk
Kitine.
Akizungumzia
chanzo cha kuporomoka kwa maadili ndani ya CCM, Dk Kitine ambaye pia
aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, alisema yalitokana na
kuanzishwa kwa makundi na mitandao ya kusaka madaraka kwenye chama.
“Mitandao
na makundi ndani ya CCM, hakikuandikishwa mahali popote. Mtandao
ulianzishwa mwaka 1995 na ulikuwa wa vijana. Mwaka huo mtandao huo
ulifanya mgomo mbele ya Mwenyekiti Ali Hassan Mwinyi na mbele ya
Mwalimu Nyerere wakati huo tunatafuta viongozi,” alisema Dk Kitine na
kuongeza:
“Wakati
Mzee Mwinyi anatuongoza kama mwenyekiti na amekuja kutueleza maazimio
ya Kamati Kuu kwamba kwanini baadhi ya wagombea hawakuwa na sifa,
wanamtandao wakasema jambo hilo halikubaliki.”
Aliongeza
kwamba, mtandao huo ndiyo umekuwa chanzo cha ufisadi ndani ya chama na
kufafanua; “Kundi hilo ndilo sasa linaendesha rushwa, linafanya
wanachama wa CCM kuwa hawana maana, linakusanya kadi. Kama wanabisha
waje kwenye kikao kama hiki wajieleze.”
Dk Kitine
alitaja kashfa za ufisadi zilizovuma kuwa ni pamoja na Deep Green,
Kagoda, Meremeta, EPA na kubainisha kwamba zote zina mkono wa kundi
hilo la mtandao.
“Lakini
yote yanatokana na kuficha matatizo, kwa mfano unapowakataza watu
kujadili suala la Muungano, unaficha nini? Sasa haya ya kuficha pia
masuala ya Kagoda na mengineyo, ipo siku watu watataka majibu yao tu
hata miaka 100 ijayo. Matokeo yake watakichukia chama,” alisema.
Kauli ya Butiku
Katika
mjadala huo, Butiku ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu
Nyerere, alisema CCM kimebadilika kutoka kuwa chama cha wakulima na
wafanyakazi na kuwa chama cha wafanyabiashara na maslahi binafsi.
“Mnapofanya
kazi katika Serikali au chama, wajibu wenu siyo kukiua chama
mlichokianzisha kama ni chama chochote au CCM kinachojiita kuwa chama
cha wakulima na wafanyakazi. Kwa bahati mbaya sana wafanyabiashara
wengi waliojiingiza katika Chama Cha Mapinduzi, wamegeuka, kazi yao na
madhumuni ndiyo yamekuwa malengo mbadala ya chama,” alisema Butiku na
kuongeza:
“Mimi
naamini biashara ni kazi, lakini kama unachukua malengo ya biashara na
kuyafanya kuwa malengo mbadala ya Chama Cha Mapinduzi, chama hicho bado
kipo?,” Alihoji.
Butiku
ambaye aliwahi kuwaandikia barua Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkapa na
Mwenyekiti wa sasa Rais Kikwete akitoa angalizo kuhusu mweleko wa chama
hicho, alisema hali ya sasa chama ni mbaya.
“Kwa hiyo
wakati ule nilisema chama kimeanza safari ya kifo. Leo ukitazama,
ukisikiliza viongozi wanavyosema, ukisiliza matendo yao, uwepo wao wote
ni wa kibiashara na si kuimarisha chama hicho, ni kuimarisha malengo
yao ya kibiashara na kibinafsi,” alisema Butiku.
Aliongeza
kuwa chama hicho kimepoteza maadili kiasi kwamba imekuwa kawaida kwa
viongozi kununua kura na kwamba siku hizi, uongozi wa chama unanunuliwa.
"Nani
anabisha kwamba CCM hatununui uongozi? CCM viongozi wote wa ngazi
mbalimbali, mmoja mmoja anieleze kama siyo kweli kwamba CCM kimekuwa
chama cha kukumbatia rushwa na kununua uongozi?,” Alihoji na
kuongeza:,Soma zaidi www.mwananchi.co.tz
Comments