Kikao cha Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF, iliyoketi kusikikiza
mashitaka dhidi ya Alhaj Ismail Aden Rage na Louis Sendeu kilifanyika
leo tarehe 24 Machi, 2012 kilisikiliza tuhuma zilizowasilishwa na TFF.
Mashitaka hayo yalihusiana na matamko yaliyotolewa na watuhumiwa hao
kabla ya mchezo wa Ngao ya Hisani kati ya Simba na Yanga, uliochezwa
tarehe 17 Agosti, 2011.
Katika mashitaka hayo, watuhumiwa hao walituhumiwa kukiuka Kanuni ya
30 (1) (f) na Kanuni ya 53 (1) (2) cha Kanuni za Adhabu za FIFA.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kutafakari maelezo hayo,
pamoja na kuchambua sheria na kanuni mbalimbali, Kamati imeamua
yafuatayo:
Hasara kwa Mdhamini
Kuhusiana na suala hasara, Kamati inaona kwamba suala hili halikuwa
na uzito wowote wala hakukuwa na hoja ya msingi, wala ushahidi wa
kuthibitisha kwamba tishio au matamko hayo yalikuwa na uhusiano na
hasara inayodaiwa kwamba mdhamini huyo aliipata. Hakuna malalamiko
yoyote yaliyotolewa kuhusiana na kinachodaiwa kuwa ni hasara
inayotokana na matamko ya viongozi hawa. Kamati imeitupilia mbali hoja
hii.
Tuhuma za matamko ya watuhumiwa
Kamati imebaini kwamba matamko hayo yalikuwa ni uvunjaji wa kanuni
na yalilenga kuchochea hisia mbaya na kuleta vurugu. Kamati ina maoni
ya kwamba viongozi wa vilabu hivi walistahili kufuata taratibu za kawaida
katika kudai haki zao, badala ya kutoa matamko ambayo yangeweza
kuchochea hisia mbaya. Kitendo hicho si cha kiungwana na kinaendana
kinyume na taratibu za uongozi wa mpira.
Wao kama viongozi, walistahili kutumia utashi na kupima athari za
matamko yao, ili kuepuka uwezekano wa kuleta msuguano usio wa lazima
na kuungiza mchezo wa mpira katika kashfa au kukosa heshima. Matamko
haya yanaweza kuwa ni kichocheo kwa viongozi wengine wenye tabia ya
namna hiyo kutumia mwanya huu kufanya vitendo hivyo.
Kwa msingi huo, Kamati inawaona wote wawili kuwa wana hatia na
matamko hayo yanayohusiana na mchezo huo. Kwa kuzingatia hilo,
Kamati inatoa onyo kali dhidi ya watuhumiwa hao wawili na inaonya
kwamba adhabu kali zaidi zitachukuliwa kama watuhumiwa watalirudia
kosa kama hili au linalofanana na hilo.
Kamati imebaini pia kwamba Mheshimiwa Aden Rage amehusika pia na
kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya Bwana Saad Kawemba wa TFF,
akidaiwa kwamba alikuwa anazuia usajili wa mchezaji Gervais Kago na
kwamba Bwana Kawemba alifanya hivyo kwa vile ana mapenzi na klabu ya
pinzani ya Yanga.
Pamoja na kwamba hakukuwa na athari za moja kwa moja dhidi ya Bwana
Kawemba, ukweli ni kwamba kitendo hicho kilikuwa ni kosa ambalo
halistahili kufanywa na kiongozi mwenye uzoefu mkubwa wa uongozi kama
Mheshimiwa Rage, na kilikuwa kina dalili za kuchochea chuki zisizo na
msingi dhidi ya Bwana Kawemba. Kitendo hicho kilikuwa kinakiuka kifungu
cha 53 (1) (2) cha Kanuni za Adhabu za FIFA.
Kamati inatoa onyo kali dhidi ya Mheshimiwa Aden Rage kwa kupatikana
na hatia yake hiyo.
Imetolewa na Kamati ya Nidhamu na usuluhishi leo tarehe 24 Machi, 2012.
..................................................
Kamishna Alfred Tibaigana
Mwenyekiti wa Kamati
Comments