Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha kawaida cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa, huko ukumbi wa Lamada jijini Dar es Salaam.Kushoto yake ni Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad akifuatiwa na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Ismail Jussa.
Mwenyekiti
wa Chama Cha Wananchi CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba amesema uamuzi wa
kumfukuza uanachama mwakilishi wa Jimbo la Wawi Bw. Hamad Rashid Mohd
ulikuwa sahihi na wala hayakuwa maamuzi magumu kama baadhi ya watu
wanavyofikiria.
Amesema Chama hicho tayari kimefanya maamuzi magumu zaidi kuliko hilo la kufukuzwa kwa Hamad Rashid na kwamba suala hilo lilifanywa kwa lengo la kukilinda chama na wanachama wake ambao wengi wao ni wanyonge.
Prof. Lipumba ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akifungua kikao cha siku mbili cha kawaida cha baraza kuu la uongozi la CUF taifa, kinachofanyika katika ukumbi wa Lamada jijini Dar es Salaam.
Amesema
Chama hicho kinazingatia na kutetea maslahi ya wanyonge, na kwamba
kitaendelea kufanya hivyo bila ya kujali maslahi ya mtu binafsi.
Prof. Lipumba pia ametoa ufafanuzi wa kiuchumi wa jinsi ya kuwaendeleza wananchi na taifa kwa jumla kwa kutumia vyema rasilimali zilizopo pamoja na teknolojia ya kisasa kwa maendeleo.
Prof. Lipumba pia ametoa ufafanuzi wa kiuchumi wa jinsi ya kuwaendeleza wananchi na taifa kwa jumla kwa kutumia vyema rasilimali zilizopo pamoja na teknolojia ya kisasa kwa maendeleo.
Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi zikiwemo ardhi yenye rutba, madini, gesi asilia, bandari na jiografia yake kwa ujumla ambapo amesema iwapo vitatumika vizuri wananchi wanaweza kunufaika na kupunguza tatizo la umaskini linalowakabili.
Amefahamisha kuwa Tanzania inapaswa kuliingiza suala la maliasili kwenye katiba na kulikabidhi kwa wananchi katika utaratibu ambao wananchi wataona kuwa ni rasilimali zao na hivyo kuweza kuzilinda.
Amesema wananchi wengi wamekuwa wakinyasisika na rasilimali zao kwa kukosa uhuru wa kisiasa na kiuchumi, na hivyo kushindwa hata kumiliki maeneo yao wanayofanyia kazi.
“Wakulima wa korosho kwa mfano hawana umiliki wa mashamba yao, hiki ni kikwazo kikubwa cha kiuchumi kwa wananchi wa vijijini.
Amewaka wazi kuwa maendeleo ya sayansi na teknolojia katika karne ya 21 ni lazima yaendane na uhuru wa kisiasa na kiuchumi kwa wananchi, na kutaka ombwe la uongozi wa serikali iliyopo liondolewe ili kurahisisha maendeleo ya kiuchumi.
“Tunahitaji tulete mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa, na hili halitowezekana ikiwa ombwe hili la utawala wa CCM wa miaka 50 tangu uhuru halijaondoka”, alisema Prof. Lipumba.
Amesema miaka 50 tangu uhuru ni kipindi kirefu ambacho baadhi ya nchi zimeweza kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi tofauti na ilivyo Tanzania, hali iliyotokana na kutokuwepo kwa mikakati madhubuti ya kukuza uchumi.
Prof. Lipumba ambaye ni mtaalamu wa uchumi na ambaye hivi karibuni alirejea kutoka nchini Marekani ambako alijikita na kazi utafiti kuhusu namna na kupanua demokrasia kwa maendeleo ya kiuchumi, amesema atatumia fursa hiyo kuitumia taaluma hiyo kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini.
Amesema inasikitisha kuona bajeti ya umeme ikiongezwa kwa kiasi kikubwa lakini tatizo linabakia pale pale, na kufafanua kuwa hakuna uwajibikaji wa kutosha katika serikali.
Prof. Lipumba pia amekemea siasa za udini ambazo amesema hazina mustakbali mwema katika kuwaunganisha watanzania na kuwaletea maendeleo.
“Watanzania waunganishwe bila kujali dini au ukabila, ili kila mtu aweze kunufaika na mpango huu wa kuwaunganisha Watanzania”, alifahamisha.
Mapema akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, amemuhakikishia Prof. Lipumba kuwa Chama kiko imara kama alivyokiwacha kabla ya kuondoka au zaidi ya hapo.
Amesema licha ya kutokea bughudha chache katika siku za hivi karibuni, lakini tayari zimetatuliwa na shughuli za Chama zinaendelea kama kawaida.
Na
Hassan Hamad Ofisi ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar
Comments