Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akifungua mkutano wa kujadili jinsi ya kuyaweka
masuala ya kinywa na meno katika hatua ya awali ya kupata huduma. Jumla
wa wajumbe kutoka nchi 18 wanahudhuria mkutano huo wa siku tatu
unaofanyika hoteli ya Courtyard jijini Dar es Salaam.
(PICHA NA IKULU)
NA MAGRETH KINABO – MAELEZO
RAIS Jakaya Kikwete amesema kwamba serikali itafanya kila iwezavyo katika kupanua na kuendesha huduma za afya zilizobora na kisasa ili kuhakikisha taifa linakuwa la watu wenye afya njema kwa kuzuia na kutibu magonjwa mbalimbali katika kipindi cha uongozi wake.
Kauli hiyo ilitolewa leo na Rais Kikwete mara baada ya kukabidhiwa kadi ,katiba na tuzo ya kukubali kuwa mwanachama wa Chama cha Madaktari wa Kinywa na Meno Tanzania na Rais wa chama hicho, Rachel Mhaville katika hoteli ya Court yard jijini DaresSalaam.
“Sikutegemea kutokea kwa kitendo hiki. Ninachoweza kusema ninaomba mniamini nitakuwa mwanachama mzuri. Tutafanyakazi kwa pamoja ili kutimiza ndoto zenu hususan kuhakikisha mradi wa kituo cha Kigamboni cha magonjwa hayo unaanzishwa.
“Hili ni jukumu kwangu , kwani lengo langu ni kuliacha taifa likiwa lenye watu wenye afya njema,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa serikali yake inafanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha ujenzi wa Chuo Kikuu kipya cha Sayansi za Afya na Tiba eneo la Mlongazila unafanikiwa ili kiweze kufanya kazi kabla ya mwaka 2015.
Rais Kikwete alisema chuo hicho kitakuwa na shule mbalimbali za afya na tiba.
Akifungua mkutano wa mafunzo ya siku tatu ya kuweka hatua za awali za kupata huduma za kuzuia na kutibu magonjwa hayo, Rais Kikwete alisema bado kuna safari ndefu ya kuiwezesha sekta ya huduma hiyo kuwa na rasimali watu wa kutosha wakiwemo madaktari, wauuguzi na watumishi wengine wa eneo hilo.
Rais Kikwete aliongeza kuwa sekta hiyo ina upungufu wa madakatari ukilinganisha na idadi ya watu nchini wapatao milioni 43 .
Alizitaja takwimu za madaktari wa sekta hiyo nchini kuwa wapo 518 ambapo uwiano unaonesha kuwa 1: 120,000 (yaani daktari mmoja kwa wagonjwa 120,000) wakati kwa sheria za Shirika la Afya la Dunia(WHO) 1:7500 (yaani daktari mmoja anatakiwa kutibu wagonjwa 7500).
“Serikali itaendelea kujenga uwezo kwenye hospitali na kituo cha afya, lazima ziwe na vitengo vya huduma za kinywa na meno,” alisisitiza huku akiongeza kwamba itasaidia kuanzisha na kupanunua vilivyopo na itangalia ili iweze kuanzisha hata katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
Alitoa changamoto kwa wadau wa sekta hiyo kuhakikisha kuwa huduma za magonjwa hayo zinapatiakana, kutolewa katika hatua za awali na kwa gharama nafuu.
Naye
Rais wa chama hicho, Mhaville alisema aliitaka jamii kuacha kutembea na
magonjwa hayo badala yake wafike hospitali ili kupata ushauri na tiba kwa kuwa magonjwa hayo yanazuilika.
Alisema changamoto iliyopo kwao ni kutoa elimu kwa jamii hususan kwenye maeneo ya vijijini.
Mhaville alisema mkutano huo utatengeneza mwongozo wa mamna ya kuyashughulikia magonjwa ya afya ya kinywa na meno, ambapo Rais alisema serikali inausubiri kwa hamu.
Comments