Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kutoa msaada wa hali na mali kwa
ajili ya kuziwezesha Asasi za kiraia zitazotoa elimu ya uraia kuhusu
katiba na kuhamasisha jamii kujitokeza katika mchakato wa zoezi zima la
upatikanaji wa katiba mpya.
Wito
huo umetolewa leo na Mjumbe wa Baraza la Katiba Zanzibar ambaye pia ni
Mwanasheria wa kujitegemea Awadh Ali Said huko katika ukumbi wa Zanlink
Majestic alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na
maoni ya Baraza hilo juu ya Sheria ya mabadiliko ya katiba No. 8 ya
mwaka 2011
Amesema
kama Serikali itakuwa tayari juu ya jambo hilo Asasi hizo zitatekeleza
jukumu la kuwahamasisha wananchi ili waweze kufanya maammuzi sahihi
katika kutoa maoni yao juu ya mchakato wa katiba mpya.
Mwanasheria
huyo amesema jamii inapaswa ishirikishwe kwa upana wake katika mchakato
wa Katiba ili ukubalike na kuridhiwa na wananchi jambo
litakalowapelekea wasijione wametengwa katika maandalizi ya mchakato huo
Amesema
ni muhimu pia kuwepo kwa mjadala wa kitaifa juu ya sheria hiyo ili
kujenga mwafaka wa kitaifa katika jambo lililo muhimu katika uhai wa
taifa.
Kuhusu
muundo wa tume Awadh alisema uteuzi wa Wajumbe wa Tume hiyo ni vyema
wajumbe wake wapate ridhaa ya Baraza la Wawakilishi au Bunge la Jamhuri
ya Muungano vyombo ambavyo ni viwakilishi halali vya wananchi na hivyo
kuondoa hofu kuwa tume hiyo imetawaliwa na kiongozi fulani
Aidha
amependekeza wajumbe wa tume waendelee kubaki katika Bunge maalum hata
baada ya Mwenyekiti wake kuwasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge hilo
ili waweze kutimiza wajibu wa kutoa ufafanuzi pale itakapostahiki.
Akielezea
kuhusu kipengele cha Muungano Mwanasheria huyo alieleza kuwa kifungu
cha 9(2) cha hadidu za rejea hakiweki wazi majadala wa Muungano na
hivyo kupendekeza kuwepo uwazi juu ya mjadala wa Muungano
Aidha
Mwanasheria huyo alipendekeza Bunge Maalum la Katiba kutokuwa na utashi
wa kisiasa wa kivyama na badala yake wajumbe wa baraza hilo wajali
maslahi ya taifa na siyo itikadi za vyama vyao katika kupata katiba
mpya.
Comments