KUUZWA KWA TIMU YA SMALL KIDS
Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana Desemba 30
mwaka jana ilijadili masuala mbalimbali yaliyofikishwa mbele yake
ikiwemo malalamiko juu ya kuuzwa kwa timu ya Small Kids ya Rukwa.
Usikilizaji
wa suala hilo uliahirishwa na Kamati kuagiza kwanza ipatiwe vitu
vifuatavyo; Katiba iliyosajiliwa ya Small Kids, muhtasari (minutes) na
uamuzi wa kikao chochote kilichofanyika kuzungumzia mauzo ya timu hiyo
ambayo iko daraja la kwanza.
Pia Kamati inataka ipatiwe
mawasiliano (correspondences) yote yaliyofanyika kuhusiana na
ununuzi/mauzo ya timu hiyo. Hivyo suala hilo litasikilishwa katika
kikao kingine cha kamati baada ya kuwasilishwa nyaraka hizo.
MGOGORO WA UONGOZI TAREFA
Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji itatuma wajumbe wake wawili
Tabora kukutana na Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Tabora (TAREFA).
Wajumbe hao katika kikao chao na
Kamati ya Utendaji ya TAREFA watasikiliza kuhusu kiini cha mgogoro
uliopo na baadaye watawasilisha taarifa kwa Kamati ya Sheria, Maadili
na Hadhi za Wachezaji. Kamati itafanyia kazi ripoti hiyo kabla ya
kufanya uamuzi.
MAREKEBISHO YA KATIBA ZA WANACHAMA
Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji pia ilifanyia kazi suala la
marekebisho ya katiba za wanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF). Katiba hizo zimegawanywa katika makundi matatu; katiba
za wanachama wapya, katiba ambazo tayari zimerekebishwa na katiba
ambazo hazijarekebishwa.
Maelekezo ya Kamati ni kuwa
itatoa mwelekeo (roadmap) utakaoonesha muda wa mwisho (deadline) wa
kufanya marekebisho kwa makundi yote hayo matatu ambapo kwa wanachama
watakaoshindwa hawataruhusiwa kuingia kwenye Mkutano Mkuu wa TFF.
Maeneo
ya msingi ya marekebisho ni sifa za uongozi. Katiba zote za wanachama
wa TFF kwa upande wa sifa za uongozi ni lazima ziwe sawa. Maeneo
mengine ni kuainishwa wazi kwa majukumu ya Kamati ya Utendaji, Mkutano
Mkuu na namna ya kutatua migogoro ya wanachama ili kuepuka watu kwenda
mahakamani.
Comments