Na Khadija Khamis –Maelezo 30/01/2012.
Mjumbe wa Baraza la Katiba Zanzibar na Mwanasheria wa kujitegemea Ali
Saleh amewashauri Wananchi wa Zanzibar kuwa makini katika kuwasilisha
maoni yao ya kutetea maslahi ya Zanzibar na sio kuburuzwa na Wanasiasa
ambao wanajali zaidi maslahi yao.
Ushauri huo ameutoa wakati alipokuwa katika mdahalo wa kujadili dhana
nzima ya marekebisho ya Katiba na Wananchi wa Mkwajuni Wilaya ya
Kaskazini A Unguja.
Mjumbe huyo alisema kuwa ndani ya mjadala wa Katiba kuna mambo
mengi ya kujadiliwa lakini kwa upande wa Zanzibar la muhimu zaidi ni
kujadili kero za Muungano kwani hii ndio nafasi pekee ya kuwakilisha
mambo yanayowayima fursa Wazanzibar.
Akifafanua zaidi alisema kuwa suala la Muungano ndio muhimu kwa
Wazanzibari kwa sababu limewaunganisha na sehemu ya pili ya Muungano
ambapo kuwekwa sawa kwake kutaleta mabadiliko makubwa ya Kisiasa na
Kiuchumi kwa Zanzibar
Alieleza kuwa kila siku jamii inazungumzia kero za Muungano jambo
ambalo si sahihi kwani Muungano si kero ila Katiba iliyopo ina upungufu
mengi ambayo yamepelekea kushindwa kukidhi haja kwa wakati na
matumaini ya watu wa pande mbili za muungano huo.
Hata hiyo alisema pindipo Wazanzibari watakaa pamoja na kujadili kwa
kina Katiba iliyopo kutawezesha mapungufu yaliyomo kuonekana jambo
litakalowapelekea kufanya maamuzi bora zaidi wakati wa kupiga kura za
maoni utapofika
Kwa upande wa Wananchi waliohudhuria kongamano hilo walisema kuwa
umefika wakati wa kujenga mustakabali mpya wa mashirikiano ya pamoja
na kuondoa itikadi za vyama kwa lengo la kujenga heshima ya Nchi ya
Zanzibar.
“Tushikamane Wazanzibar tusipokuwa pamoja Zanzibar inakwenda zake
lazima tuwe na msimamo mmoja bila kujali itikadi za vyama vyetu”alisema
mmoja wa wananchi hao
Pia waliitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iwashughulikie katika
kuwapatia vitambulisho vya Mzazibar Mkaazi ili kuweza kupata haki zao
bila ya usumbufu.
Aidha walitoa wito kwa Serikali kuzidisha juhudi za kutoa elimu sahihi kwa
Wananchi wa Zanzibar juu ya dhana ya marekebisho ya Katiba mpya ili
wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba wawe na uelewa mpana.
Idara ya Habari MAELEZO-ZANZIBAR
Comments