PRESS RELEASE
Punguza Matumizi ya Posho SIYO Matumizi ya Reli, Barabara, Elimu na Afya
Mwezi
Disemba mwaka 2011 Waziri wa Fedha na Uchumi alimwandikia barua
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) kumwahidi mambo yepi
Serikali ya Tanzania itafanya ili kurekebisha Bajeti yake. Utaratibu
huu hufanyika kila mwaka kupitia mpango unaoitwa ‘Policy Support
Instrument (PSI). Katika barua hiyo Waziri wa Fedha wa
Tanzania ameahidi kwamba Serikali itafanya juhudi kupunguza matumizi
ili kuweza kupunguza uwiano wa nakisi ya Bajeti na Pato la Taifa
(fiscal deficit to GDP ratio) kutoka asilimia 7.2 mpaka asilimia 6.6 ya
Pato la Taifa.
Waziri
wa Fedha na Uchumi ameiambia IMF kwamba ifikapo mwisho wa Mwezi
Disemba mwaka 2011 (wiki mbili zilizopita) Baraza la Mawaziri la
Tanzania limefikia maamuzi ya kupunguza nakisi ya Bajeti kwa kiwango
kilichotajwa. Maeneo yanayotajwa ni Pamoja na Miradi ya Maendeleo
ambapo jumla ya miradi yenye thamani ya Tshs 157bn itakatwa. Waziri
wa Fedha ametaja miradi hiyo katika Ukarabati na Ujenzi wa Miundombinu.
wa Fedha ametaja miradi hiyo katika Ukarabati na Ujenzi wa Miundombinu.
Kambi
ya Upinzani Bungeni inapinga kuondolewa kwa miradi ya maendeleo ili
kupunguza matumizi ya Serikali. Kimsingi wakati kama huu ambapo hali ya
uchumi ni mbaya na vijana wengi vijijini na mijini hawana ajira
tunasisitiza umuhimu wa kutumia zaidi kwenye miradi ya maendeleo.
Punguza matumizi ya kawaida
Kambi
ya Upinzani Bungeni inarejea wito wake kwa Serikali kupunguza matumizi
ya kawaida ili kupata fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo.
Haiwezekani kamwe tukawa Taifa huru iwapo miradi yetu yote ya maendeleo
inafadhiliwa na wahisani. Kiwango kidogo tulichokiweka katika Bajeti ya
mwaka huu ndicho hicho sasa kinakatwa na hivyo miradi yote ya maendeleo
kubakia kwa wahisani ama kwa mikopo au misaada. Kiwango cha Tshs 203bn
sawa na 0.5% ya Pato la Taifa ambacho Serikali imeahidi kupunguza ni
kidogo mno na kinalenga kuumiza watumishi wa kada ya chini ya Serikali
na sio viongozi wakubwa. Bajeti ya Mafunzo inayoenda kukatwa itaumiza
Manesi na Walimu au watumishi wanaoongeza ujuzi ili kuboresha kazi zao.
Serikali ikate matumizi yote yasiyo ya lazima na hasa posho
(360bn), ipunguze matumizi ya magari na yale yasiyo na uhitaji yapigwe
mnada na viongozi wote isipokuwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu,
Spika na Jaji Mkuu washushwe madaraja ya kusafiria kwenye ndege. Safari
zote ambazo hazina mahusiano na miradi ya maendeleo zipigwe marufuku
kwa muda wote wa miezi sita ya Bajeti iliyobakia.
Serikali
ihakikishe matumizi katika Sekta ya Elimu na Afya hayakatwi kabisa ili
kuhakikisha tunalinda mafanikio kiduchu ya upanuzi wa sekta hizi na
kuongeza uwezo wa Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi hasa wa
vijijini.
Matumizi ya Maendeleo yasiguswe, yaongezwe
Tayari
imeonekana kwamba katika kipindi chote cha nusu ya Bajeti Halmashauri
za Wilaya hazijapata fedha za maendeleo. Mfano Halmashauri ya Wilaya
Kigoma imepata asilimia 0.3 tu ya Bajeti ya Maendeleo ilhali
Halmashauri ya Mji wa Mpanda imepata asilimia 4 tu. Ni dhahiri miradi
ya maendeleo kwa maeneo mengi ya vijijini itakwama kwani ni wazi
kabisa kwamba Halmashauri hazipati fedha zote za Bajeti ya Maendeleo.
Serikali itambue kwamba miradi ya maendeleo sio anasa bali ndio vyanzo
vya baadaye vya mapato ya serikali. Miradi ya maendeleo hutoa ajira kwa
wananchi na hivyo kuwapunguzia umasikini wa kipato. Jumla ya Tshs 157bn
zinazotakiwa kukatwa zisikatwe bali ziongezwe ili kupata fedha za
kurekebisha miundombinu kama Reli ya Kati.Kwa mfano Reli ya Kati
inahitaji Tshs 200bn katika kipindi cha miaka 3 ili iweze kusafirisha
mizigo tani 1.5m kwa mwaka kila siku na kuzalisha faida.
Ongeza Mapato ya Ndani
Inashangaza
kwamba katika mpango wa Serikali kupunguza nakisi ya Bajeti
mkazo umewekwa kwenye kuondoa miradi ya maendeleo badala ya kuongeza
mapato. Nakisi hupunguzwa ama kwa kupunguza matumizi au kwa kuongeza
Mapato. Serikali katika Taarifa yake kwa IMF imeibua njia moja tu ya
kuongeza mapato, kodi ya mapato kutoka Kampuni ya Geita Goldmine. Huu
ni uvivu wa kufikiri.
Serikali
imeambiwa mara kadhaa suala la kuanza kutumika kwa sheria mpya ya
madini kwa Kampuni za Madini zilizokuwapo. Makusanyo ya Mrahaba peke
yake kwa sheria mpya, kiwango kipya na kanuni mpya ya kukokotoa
ingeongeza mrahaba mpaka Tshs 203bn kutoka Tshs 99bn za sasa. Kwanini
Serikali ianvuta miguu katika kutekeleza hili? Waziri wa Nishati na
Madini aliahidi Bungeni kwamba mazungumzo na Kampuni za Madini
yanaisha Mwezi Septemba. Mbona Serikali imekuwa BUBU katika hili?
Serikali
iliahidi kuangalia suala la mauzo ya mali za makampuni zilizoko
Tanzania na kodi ambayo tunapaswa kukusanya, Serikali imekuwa kimya
kabisa katika suala hili. Marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT) kwa kuondoa msamaha kwenye ‘deemed capital goods
yangeongeza mapato ya Serikali kwa kiwango kikubwa na kupunguza mzigo wa
misamaha ya Kodi.
misamaha ya Kodi.
Uwajibikaji kwa Bunge
Inashangaza
zaidi kwamba sasa imekuwa ni mtindo kwa Serikali kutoa
‘commitments’ muhimu za kibajeti kwa Shirika la IMF badala ya wananchi
kupitia Bunge. Bunge limepitisha Bajeti, mapitio yeyote ya Bajeti
yanapaswa kuidhinishwa na Bunge. Bila kufanya hivyo maana ya Bunge
kupitisha Bajeti inakuwa haina mantiki na uhuru wa Taifa letu unakuwa
haupo kwetu.
Umuhimu
wa Bunge kutunga haraka Sheria ya Ofisi ya Bajeti ya Bunge
(Parliamentary Budget Act) sasa unaonekana waziwazi. Muswada
umewasilishwa Bungeni na Wabunge binafsi kutaka kuundwa kwa mfumo wa
kuisimamia Serikali katika Bajeti. Ofisi ya Spika wa Bunge ihakikishe
muswada huu unachapishwa katika Gazeti la Serikali mara moja ili
usomwe kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Sita wa Bunge na kutungwa
kuwa sheria katika mkutano wa Saba.
Kambi
ya Upinzani inaitaka Serikali ilete mpango wa kupunguza matumizi
Bungeni ili ujadiliwe na kuidhinishwa na Bunge kabla ya kuanza
kutumika. Vinginevyo Mpango wa Serikali kwa IMF utakuwa ni kudharau
wananchi na kuuza uhuru wetu kwa Shirika la Fedha la Kimataifa. Mwalimu
Nyerere aliwahi kusema mwishoni mwa miaka ya Sabini ‘toka lini
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limekuwa Wizara ya Fedha ya
Kimataifa (International Ministry of Finance)?’
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Waziri Kivuli Fedha na Uchumi
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni (NKUB)
Dar es Salaam, 10 Januari 2012.
Comments