[Daktari
Mstaafu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Bushiri Tamimu akiandika
ripoti za wagonjwa ambao ni watoto waliolazwa wodi namba 37 katika hiyo
baada ya kuwapatia huduma jana. Hospitali hiyo imewarudisha baadhi ya
madaktari kwa mikataba kutokana hali mbaya iliyokuwa ikiendelea hapo
kutokana na mgomo wa madakari.Picha na Venance Nestory ]
Tuesday, 24 January.2012
HUDUMA MOI ZASITISHWA, WAGONJWA WARUDISHWA NYUMBANI, UONGOZI WADAI HALI NI SHWARI
HUDUMA
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jana zilizorota kutwa nzima
kutokana na mgomo wa madaktari nchi nzima uliotangazwa juzi jioni na
kuanza jana huku uongozi wa hospitali hiyo ukisisitiza kuwa huduma
zilikuwa zikiendelea kama kawaida.
Mbali
na hospitali hiyo, mgomo huo pia uliripotiwa kuathiri utoaji wa huduma
katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road huku huduma zikiendelea kama
kawaida katika hospitali nyingine karibu zote nchini.
Idara zilizoathirika zaidi na mgomo huo Muhimbili ni katika kitengo cha Tiba ya Mifupa (Moi) na Idara ya Wagonjwa wa Nje (OPD).
Tangu
saa 12:30 asubuhi, idara hizo na wodi mbalimbali zilikuwa na msongamano
wa wagonjwa hasa Moi, huku wagonjwa wa nje waliokuwa wamepokewa,
wakiendelea kusubiri huduma ambayo hata hivyo, haikutolewa.
Huduma katika Idara ya Wagonjwa wa Dharura ziliendelea kama kawaida.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, baadhi ya wagonjwa waliilani hatua ya madaktari
hao kugoma huku wengine wakiitupia lawama Serikali kwa kile
walichoeleza kuwa ndiyo chanzo cha adha hiyo.
Mmoja
wa wagonjwa walioathirika, Damian Mselea ambaye kwa sasa anaishi
Kimara, Dar es Salaam alisema alikuwa akipata matibabu katika Hospitali
ya Rufaa ya KCMC Moshi kabla ya kuhamishiwa Moi.
“Nimesafiri
kutoka Moshi nikiwa na ndugu zangu na nilipofika leo (jana),
wakalazimika kuniwahisha ili niweze kupata huduma ya matibabu, lakini
hadi sasa sielewi nini kinaendelea,” alisema Mselea akiwa ndani ya gari
la ndugu yake akiwa ameshakaa humo kwa zaidi ya saa saba bila ya kupata
huduma.
Mgonjwa
mwingine, Salome Raphael (64), mkazi wa Kinyerezi, Dar es Salaam ambaye
alifika Moi kupata tiba ya mguu wake uliovunjika alisema: “Nimefika
asubuhi na kuambiwa na watu wa mapokezi niende ofisi ya madaktari
nikaangalie kama wapo kisha nirudi mapokezi ili waniandikie niende
kumuona daktari.”
Alisema
kwa kawaida, mgonjwa kabla ya kumuona daktari huanzia mapokezi na baada
ya kuandikisha maelezo ndipo huelekezwa chumba cha daktari.
Kwa
upande wake, Rehema Mohamed wa Madale, Dar es Salaam ambaye alifika Moi
kutolewa nyuzi katika jeraha lake la mguu alisema licha ya kukaa wodini
kwa muda mrefu hakuweza kumwona daktari na wala hakukuwa na dalili
yoyote ya kuonana naye.
Vurugu OPD
Wakati
wagonjwa hao wakiendelea kusubiri huduma, eneo la OPD nusura ligeuke
uwanja wa mapambano baada ya wagonjwa waliofika kupata huduma za
kliniki, kukosa tiba na kuanza kudai fedha zao.
Wagonjwa hao na ndugu zao walisema kuwa wanapaswa kurudishiwa fedha zao walizolipa kujiandikisha kwa kuwa hawakuwaona madaktari.
Hata
hivyo, wagonjwa na watendaji katika eneo hilo walifikia mwafaka baada
ya kukubaliana kupangiana tarehe nyingine za kwenda kuonana na daktari
kwa fedha walizokuwa wameshatoa.
Mmoja
wa wagonjwa hao, Willy Rwehumbiza alisema mgomo huo umemuathiri kwa
ametokea mbali kufuata huduma za kliniki ambazo ni kila baada ya miezi
sita.
“Sina
ndugu, nimetoka Bukoba Mkoa wa Kagera, ni mfanyakazi katika Idara ya
Elimu na nina matatizo ya moyo, kitendo hiki kimeniathiri sana, sijui
itakuwaje” alisema akiwa kwenye foleni ya kwenda kupangiwa tarehe
nyingine.
Mgonjwa
mwingine, Flora Roman alilalamikia kupangiwa kurejea Machi 27, mwaka
huu... “Hii ni hatari, sisi tutakufa sasa, leo nimekuja nimekosa huduma
napangiwa Machi 27, hii si hatari! Tutafika kweli?.”
Kwa
upande wake, mgonjwa Theresia Mapunda wa Kimara, Temboni Dar es Salaam,
alisema alifanyiwa operesheni Septemba mwaka jana na alipangiwa na
daktari kurejea kwa uchunguzi kila mwezi lakini.
“Nimeshangazwa
na hutua hii. Kila mwezi nakuja kufanyiwa uchunguzi, leo nimekuja
Sh5,000 wamechukua na nimepangiwa kurudi Machi 27,” alisema Mapunda.
Waokoa jahazi
Wakati
madaktari wakiwa katika mgomo, habari zilizopatikana zimesema waliokuwa
wanaendelea kufanya kazi katika vitengo mbalimbali hospitalini hapo ni
madaktari walio kwenye mkataba na wanafunzi waliotoka chuoni.
Hata
hivyo, eneo lililokuwa likiendelea kutoa huduma katika Taasisi ya Moi
ni la wagonjwa wa dharura pekee ambalo mmoja wa madaktari alisema
wameona ni vyema kutoa huduma hapo kwa sababu wanaofikishwa ni wagonjwa
wenye mahitaji ya haraka.
Licha
ya kuwapo kwa hali hiyo, Ofisa Habari Mwandamizi wa Hospitali hiyo,
Aminiel Aligaeshi aliwaambia waandishi kuwa madaktari wanaendelea na
kazi na hakuna hata mmoja anayegoma.
“Hapa kazi zinaendelea kama kawaida, wagonjwa wanatibiwa oneni wenyewe” alisema Aligaeshi.
Alisema hospitali hiyo ya taifa ina madaktari 248 na madaktari walio katika mafunzo ya vitendo 174 na kwamba wote wako kazini.
Ofisa huyo aliwatembeza waandishi wa habari katika moja ya wodi hospitalini hapo kujionea hali halisi.
Hata
hivyo, ofisa huyo alikataa kuwapeleka waandishi katika kitengo cha OPD
ambako ndiko kulikokuwa na idadi kubwa ya wagonjwa waliokuwa wakisubiri
huduma akisema: “Muda umekwisha si mmeshaona watu wanafanya kazi!”
Mgomo wayeyuka
Hata
hivyo, wakati mgomo huo ukifanikiwa Muhimbili, huduma katika hospitali
nyingine kubwa nchini zikiwamo Temeke, Ilala, Mwananyamala na Hospitali
za mikoa ya Tanga, Dodoma, Iringa, Shinyanga, Arusha, Mara na
Kilimanjaro ziliendelea kama kawaida.
Madaktari
katika Hospitali za Mount Meru, Bugando, Bombo, Hospitali Teule ya
Muheza, Korogwe na Bunda waliendelea na kazi. Madaktari katika
Hospitali za Magunga na Bombo mkoani Tanga walisema wanasubiri kwa hamu
maagizo kutoka kwa viongozi wao ili nao wagome kuishinikiza Serikali
ili isikilize kero zao.
Katibu
Mkuu wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda, Billy Kinyaha alisema
hakuna mgomo wowote kauli iliyothibitishwa pia na baadhi ya wagonjwa
waliolazwa katika hospitali hiyo.
Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Samson Winani alisema hakuna mgomo wowote
uliofanyika: “Sisi huku hatujagoma. Wanaogoma ni wa huko Dar es Salaam.”
Katika
Hospitali ya Mount Meru, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo ya Mkoa wa
Arusha, Dk Omar Chande amesema madaktari wote jana walikuwa wakichapa
kazi. Hata hivyo, hakuna daktari aliyekuwa tayari kueleza ni kwa nini
hawakutekeleza maagizo ya kugoma kuanzia jana.
CUF walia na mawaziri
Katika
hatua nyingine, Chama Cha Wananchi (CUF), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete
kuwawajibisha Waziri wa Afya, Dk Haji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy
Nkya kwa kile kilichodai kuwa wameshindwa kutatua tatizo hilo.
Katika
taarifa yake iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, chama hicho
kilisema mbali na viongozi hao wa kisiasa, Rais pia anapaswa
kuwawajibisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Blandina Nyoni na Mganga Mkuu
wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa.
“CUF
tunamtaka Rais Kikwete kuwawajibisha wote kuanzia waziri, naibu waziri,
katibu mkuu, mganga mkuu wa Serikali, ambao wote ni wahusika wa Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwa kufanya kazi kwa dharau,” ilisema
sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Naibu Mkurugenzi wa Habari
Uenezi na Haki za Binadamu, Amina Mwidau.
Habari
hii imeandikwa na Geofrey Nyang’oro, Aidan Mhando, Gedius Rwiza,
Burhani Yakub na Raisa Said, Tanga; Ahmed Makongo, Bunda; Mussa Juma,
Arusha na Sheilla Sezzy, Mwanza.www.mwananchi.co.tz
Comments