NI
mtuhumiwa mmoja tu ambaye amesalia mahabusu kati ya watuhumiwa 20
walioshtakiwa katika kashfa ya wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya
Nje (EPA), baada ya Farijala Hussein kutimiza masharti na kuachiwa huru
jana.
NI mtuhumiwa mmoja tu ambaye amesalia mahabusu kati ya watuhumiwa 20
walioshtakiwa katika kashfa ya wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya
Nje (EPA), katika Benki Kuu (BoT) baada ya Farijala Hussein kutimiza
masharti na kuachiwa huru jana.
Masharti yaliyokuwa yakimzuia kutoka mahabusu ni pamoja na kuwasilisha
hati ya mali yenye thamani ya Sh500 milioni. Kutoka kwake sasa
kunamfanya kaimu katibu wa BoT, Imani Mwakosya kusalia pekee mahabusu.
Mwakosya anaendelea kusota rumande kutokana na kushindwa kutimiza
masharti ya dhamana ambayo ni pamoja na kutoa fedha taslimu
Sh104milioni.
Katika kesi hiyo, Maranda na mwenzake wanadaiwa kuiba zaidi ya Sh2.2
bilioni baada ya kughushi na kuwasilisha hati ya uongo katika Benki ya
Biashara na kujipatia kiasi hicho cha fedha toka BoT.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa Septemba 8 mwaka 2005 waliwasilisha hati
ya uongo kutoka Kampuni ya B Gracery and Co. Ltd ya Ujerumani na
kampuni ya Money baada ya kuonyesha kampuni hizo zilikuwa zimesajiliwa
na kwamba wao ndiyo walikuwa wakurugenzi.
Katika hatua nyingine kwa mara nyingine kesi ya wizi wa mabilioni ya
fedha EPA inayomkabili mfanyabiashara na kada wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Rajabu Maranda na mwenzake Farijala Hussein, jana haikuweza
kusikilizwa.
Kesi hiyo namba 1163, ambayo ilikuwa isikilizwe katika hatua ya awali
(Preliminary Hearing-PH) mbele ya Hakimu Anyimilile Mwaseba, jana pia
haikuweza kusikilizwa baada ya wakili wa washtakiwa hao, Mark Anthony
kushindwa kufika mahakamani na hivyo Hakimu Hezron Mwankenja
kuiahirisha.
Hiyo ni mara ya pili kwa Wakili Anthony kushindwa kufika mahakamani
hapo kwa ajili ya kesi hiyo baada juzi pia kushindwa kufika kutokana na
kile kilichoelezwa baadaye na Maranda, ambaye ni mshtakiwa wa kwanza
katika kesi hiyo, kuwa wakili huyo alikuwa na kesi nyingine Mahakama
Kuu.
Kutokana na hali hiyo, kesi hiyo iliahirishwa hadi Januari 21 mwakani itakapoendelea tena mahakamani hapo.
Katika hatua nyingine, kesi nyingine namba 1172 inayowakabili ndugu
wawili, Jay Somani na Ajay Somani, jana iliahirishwa hadi Januari 13
itakapokuja tena mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa kwa kuwa
upelelezi bado haujakamilika.Chanzo ni Gazeti la Mwananchi.
Comments