Na Masoud Sanani, Zanzibar
ABIRIA wanaosafiri kwa vyombo
vya baharini kati ya Zanzibar, Bara na Pemba kuanzia sasa wanapaswa kuwa
na vitambulisho kabla ya kuuziwa tiketi za kusafiria.
Waraka
uliotolewa na Mamlaka ya Usafiri na Vyombo vya Baharini ya Zanzibar
(ZMA), unaeleza kwamba wasafiri wote lazima waonyeshe vitambulisho ndipo
wauziwe tiketi za safari zao.
“Kuanzia Jumatatu ya tarehe 13
Agosti, 2012 abiria wote watakaonunua tiketi za kusafiria za vyombo vya
baharini lazima wawe na vitambulisho vinavyoonyesha taarifa zake
muhimu,” unasema waraka huo wa Agosti 10, mwaka huu.
Waraka huo umevitaja
vitambulisho vinavyotakiwa kuwa ni kitambulisho cha Mzanzibari, leseni
ya udereva, kadi ya benki, vitambulisho vya kazi, pasi ya kusafiria,
barua ya Sheha na kadi za ZSSF/NSSF na Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii.
Mwandishi wa habari hizi
alimshuhudia mwananchi mmoja akitaka tiketi jana na kuelezwa kuwa,
lazima awe na kitambulisho naye akajibu kuwa ana kitambulisho cha
kupigia kura na wauzaji wakasema watampa tiketi japokuwa waraka huo
haukukitaja kitambulisho hicho.
Comments