Usain Bolt usiku wa Alhamisi
alifanikiwa kuwa mwanariadha wa kwanza katika historia ya michezo ya
Olimpiki, kuweza kuutetea ubingwa wake kikamilifu katika mbio zote
fupi, mita 100 na vile mia 200.
Bolt aliwaongoza wanariadha wenzake kutoka Jamaica katika kunyakuwa medali zote tatu katika mashindano hayo ya mita 200.Muda wa Bolt katika mashindano hayo ulikuwa ni sawa na ule wa Michael Johnson katika mashindano ya Atlanta, na uliokuwa muda bora zaidi wa dunia wakati huo, wa sekunde 19.32.
Mwanariadha ambaye hufanya mazoezi na Bolt, Yohan Blake, alipata medali ya fedha, huku Warren Weir akichukua ya shaba.
Blake alikuwa amemshinda Bolt katika mashindano ya Jamaica ya kufuzu kushirikishwa katika mbio za London, lakini Blake hakuwezana na kasi ya Bolt wakati huu.
"Hili ndilo jambo ambalo nililitaka, na nimefanikiwa kulipata. Ni fahari kuu kwangu," mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 25 aliielezea BBC.
"Baada ya msimu mgumu, nilifika hapa na kufanikiwa. Nilidhani kuvunja rekodi iliwezekana. Nafikiri nilikuwa kasi, lakini sikuwa katika hali nzuri ya kuridhisha."
"Nilihisi mgongo wangu ulilemewa kidogo, kwa hiyo kile nilichofanya kujaribu kuendelea kwa kadri. Mimi ninazingatia kazi yangu sana, na michezo ya London ilikuwa ni muhimu sana kwangu."
Comments