MSIBA wa aliyekuwa staa wa muvi za Kibongo, Steven Kanumba umeanza upya kwenye Kijiji cha Izigo, Muleba, Kagera baada ya mama mzazi wa marehemu, Flora Mtegoa kuupeleka msiba huo huko sanjari na mchanga wa kaburi la Dar.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa, mama wa Kanumba alisema tangu kifo cha mwanaye hakuwahi kupeleka msiba kijijini kwake kama mila na desturi zinavyotaka.
Aliongeza kuwa hiyo yote ilitokana na kukosa muda kwani licha ya mazishi, bado watu mbalimbali kutoka nje na ndani ya nchi walikuwa wakiendelea kumiminika nyumbani kwake kwa lengo la kumfariji.
Alisema kuwa alipofika Kagera, alipokelewa na umati wa waombolezaji na msiba ulianza upya, jambo ambalo hakulitarajia.
“Nilipofika kijijini nilipokelewa na ndugu, jamaa na marafiki, kwa kweli msiba ulianza upya. Sikutarajia, watu walilia na kuomboleza,” alisema mama Kanumba.
Akaongeza: “Kwa kweli kutokana na hali ilivyokuwa, hata mimi mwenyewe nilijikuta nalia sana. Nilihisi siku hiyo ndiyo mwanangu alifariki dunia rasmi kwa jinsi watu walivyokuwa wakiomboleza.
Akaongeza tena: “Ilibidi tufanye mambo ya mila na desturi za Wahaya zikiambatana na kuzika mchanga niliouchota kwenye kaburi la Dar (Kinondoni).
Mama Kanumba alisema anamshukuru Mungu walizika salama (mchanga) na kwamba muda si mrefu alitarajia kurejea jijini Dar kutoka kwenye msiba huo.
“Namshukuru Mungu tumezika salama kwa kweli, mimi mwenyewe naendelea vizuri huku nikinywa dawa za Kihaya, nakaribia kurudi Dar hivi karibuni,” alisema mama Kanumba.
Steven Charles Kanumba alifariki dunia Aprili 7, mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa madai ya kusukumwa na Elizabeth Michael ‘Lulu’ ambaye anashikiliwa na vyombo vya dola.
Comments