Na Rajab Mkasasba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuwa
matokeo ya sensa ndio yanayoipa Serikali taarifa halisi na ya kitaalamu
juu ya idadi ya watu na taarifa nyengine muhimu katika kutayarisha
mipango ya maendeleo.
Matokeo yake hutumika kutayarisha mipango ya maendeleo
Dk. Shein aliyasema hayo katika
taarifa yake aliyoitoa kupitia vyombo vya habari kwa wananchi kuhusu
umuhimu wa wananchi katika kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya
watu na makaazi itakayofanyika tarehe 26 Agosti, mwaka huu.
Kwa matiki hiyo, Dk. Shein
alieleza kuwa kujua idadi ya watu katika eneo fulani kunaiwezesha
Serikali kukadiria mahitaji ya huduma kwa wakaazi wake ambapo kinyume
chake ni kutoa huduma pungufu kwa vile hakuna takwimu sahihi ya wakaazi
hao.
Dk. Shein alisema kuwa si jambo
la kufurahisha kusikia kuwa baadhi ya watu ambao wanawashawishi watu
wengie wasishiriki katika zoezi hilo muhimu na kusisitiza kuwa wananchi
wa Zanzibar sio wageni katika zoezi hilo kwani wameshashiriki kwa
vipindi kadhaa na kupata mafanikio ambapo sensa ya mwanzo
iliyowajumuisha watu wote ilifanyika mwaka 1948.
Comments