Maelfu
ya wananchi wa Ghana jijini Accra wamehudhuria mazishi ya kitaifa ya
rais John Atta Mills aliyefariki ghafla mwezi Julai mwaka huu.
Baadhi
ya wakuu wa nchi za Afrika wapatao kumi na wanane na Waziri wa Mambo ya
Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton walihudhuria mazishi hayo
katika uwanja wa historia ya uhuru mjini Accra.
Mills
aliyeugua saratani ya koo kwa muda mrefu amefariki ikiwa imebaki miezi
mitano tu kabla ya kufanyika uchaguzi wa urais ambao angegombea tena
nafasi hiyo.Mwandishi wa BBC mjini Accra anasema kifo chake
kimewaunganisha Waghana katika majonzi. Anasema kifo hicho kilionekana
kama jaribio kwa demokrasia changa ya nchi hiyo.
Mills aliyeanza kipindi cha miaka minne ya urais mwezi Januari mwaka 2009, amerithiwa na makamu wake rais John Dramani Mahama.
Ghana
imepongezwa na jumuiya ya kimataifa kwa namna ambavyo imeshughulikia
kipindi cha mpito katika taifa hilo linalofahamika kwa siasa zake za
mgawanyiko.
Mazishi
''Leo
giza nene limetanda katika anga ya Ghana, Afrika na kwa kweli ulimwengu
mzima,'' Bwana Mahama aliuambia umati wa waombolezaji waliokuwa
wakifuatilia mazishi hayo kupitia televisheni kubwa zilizowekwa
uwanjani hapo.
''Rais
Mills alikuwa muhimu sana katika yale ambayo tumekuwa hatuna katika
siasa zetu, uzalendo, uvumilivu katika uongozi, uaminifu,'' alisema.
Mwandishi
wa BBC Vera Kwakofi anasema watu walianza kukusanyika mapema alfajiri
katika uwanja huo wakiwa wamevalia mavazi maalum ya maombolezo rangi
nyeusi na nyekundu.Machifu wengi wa kimila walihudhuria wakiwa na ngoma
zao wakipiga midundo ya ujumbe wa kuomboleza.Mbele ya wapiga ngoma
wachezaji walichezesha mikono yao kwa namna ya ishara yenye maana
maalum.
Wakati
bendi ya jeshi ilipoingia na mwili wa marehemu uwanjani, ngoma, nyimbo
za kusifu na za kishujaa zilisimama, mwandishi wetu anasema.
Filimbi
za kuomboleza zilichezwa wakati rais Mahama alipowasha moto wa ishara
ya kumbukumbu kwa marehemu, ambaye daima alitambulika kama ''Profesa au
Mwalimu'', ikiashiria taaluma yake ya muda mrefu ya ualimu, na
''Asumdwoehene'', ikimaanisha mfalme wa amani katika lugha ya Twi.
Misururu ya foleni
Kwa
muda wa siku mbili kabla maelfu ya wananchi wa Ghana walisafiri
kuelekea Accra kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Mills.Baadhi
walipanga foleni kwa saa kadhaa, wengi wao wakilia kwa uchungu, katika
mistari ya urefu wa kama kilometa kumi nje ya jengo la Ikulu mjini
Accra.
''Nimekuwa
hapa kwa saa tatu, ili kumuona, lakini tutamkumbuka sana hapa,''
mwanamke mmoja aliiambia BBC.Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani
Hillary Clinton aliwasili Ghana akitokea Nigeria siku ya Alhamisi
kuhudhuria mazishi hayo, akikamilisha ziara yake ya siku kumi na moja
ya nchi saba za Afrika.
Ikionekana
kama mfano bora wa demokrasia katika eneo hilo la Afrika, ghana
ilichaguliwa na rais wa Marekani Barack Obama katika ziara yake ya nchi
zilizo kusini mwa jangwa la sahara mwaka 2009.
Mills
aliyefariki akiwa na umri wa miaka 68 alikuwa ni mwanasiasa wa ngazi ya
juu kwa miaka mingi.Kati ya mwaka 1997-2001 alikuwa makamu wa rais kwa
aliyekuwa mtawala wa kijeshi Jerry Rawlings, lakini alijiweka mbali na
kiongozi huyo.
Comments