Baba mzazi wa mwanasoka Mbuyi Twite amemzuia mwanaye kuja nchini
kujiunga na klabu ya Yanga kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa
michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope alisema jana kuwa,
wamepata taarifa kutoka Congo kwamba baba huyo, Mzee Twite anazitaka
Simba na Yanga zikutane ili kumaliza utata uliojitokeza katika usajili
wa mwanaye.
Mzee Twite ameelezea msimamo wake huo baada ya
viongozi wa Simba na Yanga kuvutana kuhusu usajili wa mchezaji huyo wa
APR ya Rwanda.
Awali iliripotiwa kuwa, Simba ilifanikiwa
kumsajili mchezaji huyo kupitia Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden
Rage aliyekwenda Rwanda na kumsainisha mkataba, lakini baadaye zikaja
taarifa kuwa, Yanga nayo imemsajili kupitia mjumbe wake wa kamati ya
utendaji, Abdalla Bin Kleb.
Hans Pope ameilaumu Yanga kwa
kuingilia kati usajili wa Twite na kuongeza kuwa, hali hiyo inaweza
kuleta machafuko miongoni mwa mashabiki wa klabu hizo mbili.
Hans
Pope amesema kitendo cha wenzao kuwazunguka na kumshawishi Twite
kurejesha fedha walizompa ili asajili Yanga, kinaweza kuleta uhasama
usio na ulazima.
"Tumepata taarifa kuwa baba mzazi wa Mbuyu (Twite) amemkataza mwanaye kuja kuichezea Yanga kwa hofu ya maisha yake.
"Mzee
Twite anataka Simba na Yanga zikutane kufanya mazungumzo kwa lengo la
kuweka mambo sawa kisha ndipo amruhusu kuja Tanzania," alisema Pope.
"Unadhani
kwa kitendo walichofanya Yanga, mashabiki wa Simba watafurahi? Baba
yake mzazi (Twite) amechukizwa na hali hiyo, anahofia usalama wa kijana
wake," alisema Pope.
"Vita ya soka haina tofauti na ile ya
siasa au dini. Kwa hiyo baba mzazi wa Mbuyu ameomba Yanga na Simba
kumaliza suala hili mwanaye aweze kucheza soka kama ilivyo kazi yake.
"Katika
kusisitiza ukweli wa madai yao, Pope alisema tayari uongozi wa Yanga
umeomba kukutana nao ili kuzunguza na kumaliza suala hilo.
"Ukweli
ni kwamba, hatuna tatizo na Yanga. Nafikiri siyo mara yao ya kwanza
wala mwisho kutufanyia mchezo huu mchafu. Ni kawaida yao."
"Wameomba
[Yanga] tukutane ili kumaliza utata wa suala hili, vinginevyo Twite
hatakuja siyo kujiunga na Yanga au Simba, bali haji kabisa."
Aliongeza:
"Tulianza mazungumzo na Bahanuzi (Said)wakatuzunguka na kumsainisha,
ikawa hivyo tena kwa Kavumbagu (Didier) na sasa wametuma viongozi Kenya
kutaka kumsainisha Pascal Ochien ambaye yupo na timu Arusha."
"Nafikiri
Yanga kama wanataka kulipa kisasi cha mabao matano tuliyowafunga,
wacheze mpira na siyo kutuzunguka na kusajili wachezaji wetu."
"Hata
sisi tunaweza mchezo huo mchafu---ni kweli tunaweza kuwafanyia, lakini
hatuoni sababu ya kufanya hivyo," alisema zaidi Pope.
Source: Mwananchi.co.tz
Source: Mwananchi.co.tz
Comments