Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba akiongea na
waandishi wa habari ofisi za Tume leo (Alhamisi, Agosti 9, 2012) kuhusu
tathmini ya kazi ya Tume ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba
Mpya. Kulia ni Katibu wa Tume Bw. Assaa Rashid.
Mwandishi
wa Habari wa Radio Deutchelle Welle Bi. Hawra Shamte akiuliza swali
katika mkutano kati ya waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba. Mkutano huo
ulifanyika ofisi za Tume jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba avitaka
vyama vya siasa, asasi za kidini na wanaharakati kuacha kuwaelekeza
wananchi aina ya maoni wanayopaswa kutoa kuhusu Katiba Mpya.
Jaji
Warioba ameyasema hayo leo (Alhamisi, Agosti 9, 2012) katika mkutano
wake na waandishi wa habari kuzungumzia tathmini ya mikutano ya awamu
ya kwanza ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya katika
mikoa minane ya Pwani, Dodoma, Manyara, Kagera, Shinyanga, Tanga,
Kusini Unguja na Kusini Pemba.
“Sio
wanasiasa tu, watu wote wakiwemo viongozi wa kidini, wanaharakati na
taasisi zisizo za kiserikali ziache kuwalazimisha wananchi watoe maoni
wanayotaka wao. Wananchi wawe huru kutoa maoni yao,” alisema na
kuongeza kuwa vyama vya siasa, asasi zisizo za kiserikali ziatapata
muda wa kuwasilisha maoni yao Tume.
“Mwananchi
akitoa maoni yake binafsi, anakuwa ‘very articulate’ (anajieleza kwa
ufasaha), lakini akielekezwa cha kusema, na ukamuomba ufafanuzi,
anashindwa hata kueleza,” alisema Jaji Warioba katika mkutano huo
uliohudhuriwa na pia na Katibu wa Tume hiyo, Bw. Assaa Rashid na Naibu
Katibu Bw. Casmir Kyuki.
Kuhusu
idadi ya mikutano iliyofanyika katika awamu ya kwanza, Mwenyekiti huyo
amesema Tume yake imefanya mikutano 386 katika mikoa minane ya awamu ya
kwanza kwa muda wa mwezi mmoja.
“Wastani
wa wananchi 188,679 walihudhuria mikutano hiyo ya Tume. Hii ikiwa ni
wastani wa watu 489 walifika kwenye kila Mkutano,” alisema na kuongeza
kuwa Tume inaridhika na idadi hii na inaonesha wananchi wana mwamko wa
kutoa maoni yao.
Kati
ya waliohudhuria, Jaji Warioba alisema, wananchi 17,440 walitoa maoni
yao kwa njia ya kuzungumza kwenye mikutano hiyo na jumla ya wananchi
29,180 walitoa maoni yao kwa njia ya maandishi na kuyawasilisha kwenye
Mikutano ya Tume.
Jaji
Warioba aliongeza kuwa Tume ilipokea maombi na kufanya mikutano nane na
makundi maalum yakiwemo Taasisi za Dini na Vyombo vya Ulinzi na Usalama
katika awamu ya kwanza.
“Kimsingi,
Tume imeridhika na kazi ya ukusanyaji wa maoni katika awamu ya kwanza
kwani mikutano yote iliyopangwa na Tume imefanyika na imefanyika kwa
amani na utulivu na wananchi walivumiliana katika kutoa maoni yao,”
alisema.
Akizungumzia
changamoto, Mwenyekiti huyo alisema katika mikutano ya Tume, wanawake
bado hawajitokezi kwa wingi kutoa maoni yao mbele ya Tume ingawa
wanahudhuria mikutano hiyo na kusisitiza kuwa Tume itaendelea
kuwahamasisha kutoa maoni yao kwa uhuru na uwazi.
Kuhusu
kuanza kwa awamu ya pili ya mikutano ya kukusanya maoni, Jaji Warioba
alisema kazi ya kukusanya maoni kwa awamu ya pili inatarajiwa kuanza
rasmi tarehe 27 Agosti, 2012 na ratiba ya mikutano hiyo itatolewa na
Tume hivi karibuni.
Akiongea
katika mkutano huo, Naibu Katibu wa Tume hiyo, Bw. Kyuki alisema kuwa
awamu ya pili ya kazi ya ukusanyaji maoni ya wananchi kuhusu Katiba
Mpya itafanyika katika mikoa saba ambayo ni Mbeya, Morogoro, Lindi,
Ruvuma, Kigoma, Katavi na Mwanza.Inatoka kwa Mjengwa.
Comments