ASEMA ATAFANYA HIVYO BUNGE LA OKTOBA KAMA SERIKALI ITASHINDWA, MABILIONI HAYO YAHUSISHWA NA UFISADI WA MEREMETA
Mhe. Zitto Kabwe |
Waandishi Wetu
MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe ameahidi kuwataja
wanaohusika kuficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi katika kikao
kijacho cha Bunge Oktoba, mwaka huu iwapo Serikali itashindwa kufanya
hivyo hadi muda huo.
Wakati Zitto akisema hayo,
kashfa hiyo imechukua sura mpya na sasa fedha hizo zinahusishwa na
ufisadi katika Kampuni ya Meremeta.
Kauli ya Zitto ambaye pia ni
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, imekuja siku chache tangu Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kuwataka wanaowafahamu
walioficha fedha hizo kuwataja hadharani ili iwe rahisi kwa Serikali
kuwachukulia hatua.
Hata hivyo, Zitto akizungumza na
gazeti hili jana alisema: “Mimi ni mbunge makini ninayefahamu taratibu
za Bunge na kuheshimu haki za watu wengine, siwezi kukurupuka katika
suala hili. Ninaiachia Serikali na vyombo vyake iendelee kulifanyia kazi
na ikiwa watashindwa kuwataja wahusika, basi wasubiri kikao kijacho,
nitaweka hadharani majina ya wahusika wote.”
Zitto alisisitiza kuwa Serikali
ina uwezo wa kupata taarifa zozote inazozihitaji kutoka Uswisi na kwamba
ndiyo maana ameipa muda wa kulifanyia kazi suala hilo kabla yeye
hajachukua hatua ya kuwataja wahusika.
“Sikia, lazima tukubaliane jambo
moja kwamba mimi siyo Serikali, wala sina dola, ndiyo maana nasema
kwamba tusubiri utekelezaji wa ahadi ya Serikali, lakini wakishindwa
kuwataja, basi mimi nitatumia nafasi yangu kama mbunge kuwataja na
nitafanya hivyo ndani ya Bunge na wala siyo nje ya hapo,” alisema.
Uchunguzi zaidi wa gazeti hili
umebaini kuwa kiasi cha Dola za Marekani 186 milioni (takriban Sh300
bilioni) kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1,600
kwa Dola ya Marekani, kimefichwa katika benki tatu tofauti za Uswisi.
Comments