
Spika wa Bunge, Anne Makinda, ameunda kamati ndogo ya kuchunguza tuhuma za baadhi ya wabunge kuhongwa na makampuni ya mafuta.
Sakata hilo lilianza baada ya baadhi ya wabunge waliokuwa wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2012/13, kudai kuna wenzao wamehongwa na makampuni ya mafuta ili kushinikiza waziri wa wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu wake, Eliakim Maswi, wang'olewe katika nafasi zao.
Spika Makinda alitangaza kamati hiyo jana asubuhi baada ya kipindi cha matangazo bungeni.
Alisema ofisi yake imeweka hadidu za rejea kwa kamati ndogo ambazo zinalenga katika kuchunguza na kumshauri kama tuhuma kwa baadhi ya wabunge na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya rushwa ni za kweli ama hapana.
Alisema baada ya mashauriano kati yake na Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Brigedia Jenerali Mstaafu, Hassan Ngwilizi, ilionekana kuwa kwa kuzingatia uhalisia wa suala lenyewe linaweza kushughulikiwa vizuri zaidi kwa mujibu wa Kanuni ya 114 (18).
Kwa mujibu wa kanuni hiyo, Kamati yoyote inaweza kuunda kamati ndogo kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli zake, kwa kadiri itakavyoona inafaa na kila kamati ndogo itapangiwa kazi zake na kamati ya kudumu inayohusika.
Comments