Maelfu
ya raia wa Ethiopia walikusanyika katikati mwa mji mkuu Addis Ababa
jana, kuipokea maiti ya waziri mkuu wao, Meles Zenawi, ambaye alifariki
katika hospital moja mjini Brussels, Ubelgiji.
Kulikuwa na msongamano mkubwa wa
magari na watu kwenye barabara inayotoka uwanja wa ndege wa mjini Addis
Ababa kuelekea nyumbani kwa marahemu Meles Zenawi, ambako maiti yake
imewekwa ili wananchi waweze kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi wao.
Jeneza lenye mwili wa marehemu
ambalo lilifunikwa na bendera ya taifa lilisindikizwa na bendi ya jeshi,
huku wakiwepo pia wanasiasa, maafisa wakuu wa jeshi, wanadiplomasia na
viongozi wa kidini. Mke wake Azeb Mesfin ambaye alijitandia kwa mavazi
meusi ya msiba, aliisindikiza maiti ya mumewe ambayo kutoka Brussels
ilisafirishwa na shirika la ndege la Ethiopia. Baadhi ya waombolezaji
walibeba picha za Meles.
Mwisho wa minong'ono
Kifo cha waziri mkuu huyo
ambacho kilitangazwa usiku wa kuamkia jana, kilimaliza uvumi wa miezi
kadhaa kwamba kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 57 alikuwa na matatizo
makubwa kiafya. Ethiopia imetangaza kuwa taifa liko katika kipindi cha
maombolezo, lakini tarehe ya mazishi bado haijatangazwa.
Comments